KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 2, 2010

BRAZIL VS TANZANIA

MABINGWA wa zamani wa Kombe la Dunia, Brazil wanatarajiwa kutua nchini Jumapili kwa ajili ya pambano lao la kirafiki la kimataifa dhidi ya timu ya taifa, Taifa Stars.
Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, limepangwa kufanyika Jumatatu kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
Brazil inatarajiwa kuja nchini ikiwa na kikosi cha wachezaji 23 wanaotarajiwa kuichezea timu hiyo katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia, zinazotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini.
Kabla ya kuja nchini, Brazil ilitarajiwa kucheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zimbabwe. Mechi hiyo ilitarajiwa kuchezwa jana usiku mjini Harare.
Kisoka Brazil ipo juu ikilinganishwa na Tanzania. Kwa sasa, Brazil inashika nafasi ya kwanza kwa ubora wa soka duniani wakati Tanzania inashika nafasi ya 108.
Takwimu za viwango vya ubora wa soka vinaonyesha kuwa, Brazil imekuwa ikishika namba moja kwa miaka mingi, isipokuwa mwaka 1993 na 2001, ambapo ilishika nafasi ya tatu na mwaka 2008 ilipoporomoka na kushika nafasi ya tano.
Mabingwa hao wa zamani wa dunia waliporomoka hadi nafasi ya pili kati ya Januari na Machi mwaka huu kabla ya kupanda tena nafasi ya kwanza Aprili mwaka huu baada ya kuiengua Hispania, iliyoshika nafasi hiyo kwa miezi mitano.
Brazil imewahi kutwaa ubingwa wa dunia mara tano, mwaka 1958, 1962, 1970, 1994 na 2002. Imewahi kushika nafasi ya pili katika fainali za 1950 na 1998, nafasi ya tatu 1938 na 1978 na nafasi ya nne 1974. Imecheza fainali zote 18 za kombe hilo.
Brazil pia imewahi kutwaa Kombe la Copa America mara nane, miaka ya 1919, 1922, 1949, 1989, 1997, 1999, 2004, 2007 na kushika nafasi ya pili mara 11. Pia imetwaa kombe la CONCACAF miaka ya 1996 na 2003.
Kikosi cha Brazil kinachonolewa na Kocha Carlos Dunga, kilianza mazoezi kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia mwanzoni mwa mwezi uliopita huku mashabiki na waandishi wa habari wakizuiwa kuyashuhudia.
Wachezaji wanaounda kikosi cha Brazil, klabu wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Julio Cesar (Inter Milan), Doni (Roma), Heurelho Gomes (Tottenham); Maicon (Inter Milan), Dani Alves (Barcelona), Lucio (Inter Milan), Juan (Roma), Luisao (Roma), Thiago Silva (AC Milan) na Gilberto (Cruzeiro).
Wengine ni Michel Bastos (Lyon); Gilberto Silva (Panathinaikos), Felipe Melo (Juventus), Josue (Wolfsburg), Elano (Galatasaray), Ramires (Benfica), Kleberson (Flamengo), Kaka (Real Madrid), Julio Baptista (Roma); Robinho (Santos/Manchester City), Nilmar (Villarreal), Luis Fabiano (Sevilla), Grafite (Wolfsburg).
Katika fainali za mwaka huu, Brazil imepangwa kundi G pamoja na timu za Korea Kaskazini, Ivory Coast na Ureno.
Kwa upande wa Tanzania, nafasi ya juu kwa ubora wa kiwango cha soka duniani ilikuwa ya 70 mwaka 1995. Mwaka 1996 iliporomoka hadi nafasi ya 89 na mwaka uliofuata iliporomoka tena hadi nafasi ya 96.
Mwaka 1998 Tanzania iliporomoka zaidi hadi nafasi ya 118 kabla ya kufika nafasi ya 172 mwaka 2004. Ilipanda nafasi ya 89 mwaka 2007, lakini ilishuka hadi nafasi ya 99 mwaka 2008, ikashuka tena nafasi ya 106 mwaka 2009 hadi kufika nafasi ya 108 inayoshikilia hivi sasa.
Kikosi cha Tanzania kinachonolewa na Kocha Marcio Maximo, kilishindwa kufanya vizuri katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 baada ya kushika nafasi ya tatu katika kundi lake.
Katika mechi zake wa kuwania kufuzu kucheza fainali hizo, ilitoka sare ya bao 1-1 na Mauritius mjini Dar es Salaam, ikachapwa bao 1-0 na Cape Verde mjini Praia kabla ya kutoka suluhu na Cameroon mjini Dar es Salaam.
Katika mechi za marudiano, Tanzania ilichapwa mabao 2-1 na Cameroon mjini Yaounde, ikaichapa Mauritius mabao 4-1 mjini Curepipe kabla ya kuicharaza Cape Verde mabao 3-1 mjini Dar es Salaam.
Tanzania ilimaliza michuano hiyo ikiwa ya tatu kwa kuwa na pointi nane baada ya kucheza mechi sita. Cameroon ilitwaa uongozi kwa kuwa na pointi 16, ikifuatiwa na Cape Verde iliyopata pointi tisa. Mauritius ilishika mkia kwa kuambulia pointi moja.
Kabla ya kupambana na Brazil, Tanzania inatarajiwa kumenyana na Rwanda keshokutwa mjini Kigali katika mechi ya marudiano ya michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Katika mechi ya awali, Tanzania na Rwanda zilitoka sare ya bao 1-1. Matokeo hayo yanatoa nafasi kwa timu yoyote itakayoshinda keshokutwa kufuzu kucheza fainali hizo, zinazotarajiwa kufanyika nchini Libya.
Wachezaji wanaotarajiwa kuunda kikosi cha Tanzania kitakachomenyana na Brazil ni makipa Shabani Kado na Jackson Chove na mabeki Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Kevin Yondani, Nadir Haroub ‘Canavaro’.
Wengine ni Mussa Hassan Mgosi, Mrisho Ngasa, John Boko, Abdi Kassim, Uhuru Selemani, Abdulrahim Humoud, Erasto Nyoni, Shaaban Nditi, Nurdin Bakari, Kigi Makasi na Jerry Tegete.
Katika kikosi hicho, pia watakuwemo kiungo Henry Joseph anayecheza soka ya kulipwa nchini Sweden, Nizar Khalfan anayecheza soka nchini Marekani.
Japokuwa viingilio vya mechi hiyo vinaonekana kuwa ni vya juu, ujio wa Brazil nchini utasaidia sana kuitangaza Tanzania kimataifa. Mechi hiyo inatarajiwa kuonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni katika nchi 160.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela amesema wamepanga viingilio vya juu kwa sababu gharama za kuileta Brazil nchini ni kubwa.
Timu hiyo imelipiwa usafiri wa ndege wa kuileta Tanzania na kuirejesha Afrika Kusini, imepangiwa kukaa kwenye hoteli ya Movenpick na imeahidiwa kupewa ulinzi mkali kwa ajili ya wachezaji na viongozi wake.
Kiingilio cha juu katika mechi hiyo ni sh. 200,000 kwa jukwaa la VIP A. VIP B ni sh. 150,000, VIP C sh. 100,000, jukwaa la rangi ya chungwa sh. 80,000, viti vya rangi ya kijani na bluu sh. 30,000 na viti vya nyuma ya magoli sh. 50,000.

No comments:

Post a Comment