'
Thursday, June 10, 2010
Madega bado kiongozi halali Yanga
‘Madega out Yanga’, ‘Madega ang’olewa’, ‘Uchaguzi Yanga Juni 27’, ‘Jaji Mkwawa kuiongoza Yanga hadi uchaguzi’, ‘Katiba Yanga yapitishwa’.
Hivyo ni baadhi tu ya vichwa vya habari vilivyopamba magazeti mbalimbali yaliyochapishwa Juni 7 mwaka huu, ikiwa ni siku moja baada ya klabu ya Yanga kufanya mkutano mkuu maalumu wa kupitisha katiba.
Mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama wapatao 4,000 na kuendeshwa na Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega, ulifanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Karibu kila gazeti liliandika taarifa za mkutano huo kivyake. Yapo yaliyoandika kuwa, uongozi wa Madega umeondolewa madarakani na mengine yaliripoti kuwa, umesimamishwa. Vyombo vingine vilikwenda mbali zaidi kwa kuripoti kuwa, katika mkutano huo, wanachama walimteua Jaji Mkwawa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, kuchukua nafasi ya Madega hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Hali hii ilisababisha wananchi wengi kushindwa kutambua ni kipi hasa kilichotokea kwenye mkutano huo. Je, ni kweli kwamba uongozi wa Madega uliondolewa madarakani? Kwa kigezo na taratibu zipi?
Wengine walishindwa kutambua lengo hasa la mkutano huo lilikuwa lipi? Je, marekebisho ya katiba yalipitishwa? Na kama mkutano huo ulikuwa wa kujadili katiba, kwa nini wanachama walichukua uamuzi wa kumuondoa madarakani Madega?
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na uongozi wa Yanga kabla ya mkutano huo, lengo lilikuwa kujadili na kupitisha marekebisho ya katiba, vikiwemo vipengele kadhaa vilivyopendekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Na hivyo ndivyo ilivyofanyika. Baada ya Madega kuwauliza wanachama mara tatu, iwapo wameyakubali marekebisho hayo yaliyotolewa na TFF na kumjibu ndio, aliamua kufunga mkutano na kutangaza kuwa, uchaguzi mkuu utafanyika Julai 4 mwaka huu.Alifanya hivyo kwa sababu ajenda ya mkutano huo ilishamalizika.
Karibu vipengele vyote vipya vya katiba ya Yanga vilivyowasilishwa kwenye mkutano huo, vilitokana na ushauri wa TFF, isipokuwa kipengele kinachohusu Baraza la Wadhamini, ambacho ndicho kilichozua utata.
Katika mapendekezo yaliyowasilishwa na uongozi, Baraza la Wadhamini lilitakiwa kuwajibika kwa kamati ya utendaji, lakini wanachama walipinga na kutaka liwajibike kwenye mkutano mkuu wa wanachama. Katika hali ya kushangaza, mara baada ya Madega kutangaza kufunga mkutano, wanachama walianza kumzomea Madega wakidai kuwa, wamemchoka.
Ilibidi Jaji Mkwawa aingilie kati na kuokoa jahazi kwa kuamuru mkutano uendelee ili wanachama waweze kupanga tarehe ya uchaguzi. Na kwa kauli moja, wanachama walikubali uchaguzi ufanyike Juni 27 mwaka huu.
Katika maelekezo yake kwa wanachama, Jaji Mkwawa alisema, kisheria, uongozi wa Madega ulimaliza muda wake tangu Mei 29 mwaka huu na kama bado wapo madarakani, ukomo wao ni siku 40, hivyo upo uwezekano wa uchaguzi mkuu kufanyika Juni 27 au siku zingine ndani ya hizo.
Kwa mantiki hiyo, si sahihi kwa sasa kusema kuwa Madega ameondolewa madarakani. Madega bado ni mwenyekiti halali wa Yanga hadi uchaguzi utakapofanyika.
Uhalali wa Madega kuendelea kuwa mwenyekiti wa Yanga pia unatokana na ukweli kwamba, hakukuwa na hoja iliyowasilishwa kwa wanachama ya kutaka kumuondoa.
Ikumbukwe kuwa, mwenyekiti wa Yanga ndiye mwendeshaji na msimamizi wa mikutano yote ya wanachama wa klabu hiyo. Hivyo hakukuwa na uhalali kwa wanachama kumteua Jaji Mkwawa kuendesha mkutano huo kwa sababu hayo si majukumu yake.
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga, Jaji Mkwawa ni mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, hivyo majukumu yake ni kusimamia zoezi la uchukuaji fomu, kuwahoji wagombea na kuendesha uchaguzi.
Pia haiingii akilini ni vipi Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi kwa Wachezaji ya TFF, Alex Mgongolwa walihudhuria mkutano huo na kuwahutubia wanachama.
Je, ni kweli kwamba TFF inapaswa kuwatuma viongozi ama wajumbe wake kuhudhuria mikutano ya klabu zilizo wanachama wake? Kama si kweli, Nyamlani na Mgongolwa walihudhuria mkutano huo kwa mwaliko wa nani? Kama walihudhuria kama wanachama wa Yanga, kwa nini walipewa nafasi ya kuzungumza?
Kauli iliyotolewa na Nyamlani wakati wa mkutano huo pia inashangaza. Makamu huyo wa kwanza wa rais wa TFF alisema, muda wa kiongozi kuwepo madarakani unapomalizika, lazima mkutano mkuu uridhie kumwongezea muda zaidi, hata kama ni siku moja.
Lakini Nyamlani amesahau kwamba anahodhi vyeo vitatu katika vyama tofauti. Mbali na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais TFF, pia bado ni Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na Katibu wa Chama cha Soka wilaya ya Temeke (TEFA) wakati muda wa uongozi wake katika vyama hivyo umeshamalizika.
Sasa hapa ni nani anayehodhi madaraka kati ya Madega na Nyamlani?
Ikumbukwe pia kwamba, Madega na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako ndio wanaopaswa kutia saini marakebisho ya katiba ya Yanga baada ya kupitishwa na TFF. Hakuna wengine wanaoweza kufanya hivyo zaidi yao.
Sasa iweje wanachama waseme wamemuondoa Madega madarakani? Hiyo katiba itatiwa saini na nani kabla ya kupelekwa kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini ili isajiliwe?
Aidha, kama Madega ameondolewa madarakani, ni nani atakayeitisha mkutano wa uchaguzi mkuu hiyo Juni 27? Na je, uongozi mpya utakaoingia madarakani hiyo siku utakabidhiwa madaraka vipi na nani?
Jambo jingine linaloshangaza kuhusu mkutano huo wa marekebisho ya katiba ni kitendo cha baadhi ya viongozi wa TFF kuwasilisha mapendekezo mapya ya marekebisho ya katiba kwa Yanga usiku wa kuamkia mkutano huo wa Jumapili.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, Jumamosi usiku, mmoja wa viongozi wa TFF aliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Yanga maelekezo mengine ya shirikisho hilo kuhusu marekebisho ya ibara za 22 (2); 29 (4); na 61 (9) kinyume na maelekezo yao ya awali kuhusu ibara 22 (2) na 29 (4) katika barua ya TFF kumb. Na. TFF/TECH/LEP.09/04 ya Desemba 18, 2009.
Maelekezo hayo mapya ya TFF ni kuhusu muda wa mwisho wa uongozi kwa mujibu wa katiba ya 2007, ambapo awali shirikisho hilo lilitaka ibara hiyo iondolewe; pia akidi ya mkutano wa dharura, ambayo sasa itakuwa ni ½ ya wajumbe waliohudhuria badala ya maelekezo ya awali ya 2/3 ya wajumbe.
Katika maelekezo hayo mapya ya TFF ya Jumamosi usiku, mdhamini wa Yanga sasa atawajibika kwa mkutano mkuu badala ya kamati ya utendaji.
Ni kwanini TFF iliwasilisha maelekezo hayo mapya usiku wa kuamkia mkutano huo wa marekebisho ya katiba?Kama walifanya hivyo kwa shinikizo, basi ni TFF wenyewe ndio wanaofahamu na yule aliyewapa shinikizo hilo.
Kilichotokea katika mkutano huo linapaswa kuwa funzo kubwa kwa wanachama wa Yanga kwamba wasikubali ‘kupelekeshwa’ na watu wachache wenye lengo la kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi badala ya klabu. Wanapaswa kukumbuka msemo wa Kiswahili unaosema, ‘Majuto mjukuu’.
Ni dhahiri kwamba wanachama wa Yanga waliingia kwenye mkutano huo wakiwa tayari wameshaandaliwa kutenda waliyoagizwa na ‘watu’ wao. Hili ni jambo la hatari kwa mustakabali wa Yanga na endapo hawatakuwa makini, watakuja kujuta baadaye.
Inawezekana ni kweli Madega ana matatizo yake, lakini ukweli unabaki palepale kwamba, taratibu zilizotumika kumwondoa madarakani katika mkutano huo hazikuwa halali na hakuna kipengele chochote kwenye katiba ya Yanga kinachozungumzia kuwepo kwa uongozi wa muda.
Hivi kwa namna ile alivyozomewa Madega, ni mtu gani na heshima zake atakubali kugombea nafasi mojawapo ya uongozi wa Yanga? Tusubiri, tuone.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment