KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 2, 2010

Buriani Mayaula Mayoni na Mzee Pwagu


MWANAMUZIKI mkongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Fredy Mayaula Mayoni amefariki dunia.
Habari kutoka nchini Congo zimeeleza kuwa, Mayaula alifariki dunia Mei 27 mwaka huu mjini Brussels nchini Ubelgiji.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mayaula alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya ubongo, uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.
Mwanamuziki huyo, ambaye alikulia na kusoma nchini Tanzania, aliwahi kuwa mchezaji wa klabu ya Yanga miaka ya 1970.
Mayaula (68) atakumbukwa sana na mashabiki wa muziki wakati alipokuwa katika bendi ya TP OK Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na marehemu Franco Makiadi.
Moja ya vibao vilivyompatia sifa na umaarufu mkubwa kimuziki ni ‘Cherie Bondowe’, ambacho alikipiga alipokuwa TP OK Jazz.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, mwanamuziki huyo aliachia kibao kingine kikali, kinachojulikana kwa jina la ‘Mbongo’, ambacho hadi leo bado kinapigwa mara kwa mara kwenye vituo mbalimbali ya radio nchini na kumbi za burudani.
Katika hatua nyingine, mwigizaji maarufu wa michezo ya radio na filamu nchini, Rajabu Hatia amefariki dunia.
Rajabu (87), ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Mzee Pwagu, alifariki Mei 28 mwaka huu katika hospitali ya Amana mjini Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na kwikwi.
Mzee Pwagu alizikwa siku iliyofuata katika makaburi ya karibu na nyumbani kwake, Kigogo Mbuyuni mjini Dar es Salaam.
Alianza kupata umaarufu miaka ya 1970 alipokuwa akishiriki katika kipindi cha mchezo wa radio kilichokuwa kikirushwa hewani na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Alicheza michezo hiyo akiwa na marehemu Ibrahim Raha (Mzee Jongo), marehemu Ally Tajiri (Meneja Mikupuo), Zena Dilip, Theckla Mjata.
Mzee Pwagu alizaliwa mwaka 1923 mjini Tabora na kusoma shule ya Tabora Town kuanzia mwaka 1942 na baadaye kuhamishiwa shule ya Minaki ya mjini Dar es Salaam.
Katika sehemu kubwa ya maisha yake, Mzee Pwagu alikuwa akifanyakazi ya ubaharia katika meli mbalimbali hadi mwaka 1946 alipoamua kuachana na kazi hiyo na kuwa fundi mchundo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam.
Mzee Pwagu ni mmoja wa waanzilishi wa kikundi cha sanaa za maonyesho cha Kaole, ambacho kilikuwa kikiandaa tamthili mbalimbali zilizokuwa zikionyeshwa na kituo cha televisheni cha ITV.

No comments:

Post a Comment