KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 2, 2010

MBANGU NGUZA: Muziki 2010 hapana!


MWANAMUZIKI Mbangu Nguza amesema hatajihusisha na masuala ya muziki kwa mwaka wote wa 2010.
Nguza alielezea msimamo wake huo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Ben and Mai, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC 1.
Mwanamuziki huyo, ambaye ni mtoto wa Nguza Vicking, aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela alisema, amefikia uamuzi huo ili apate nafasi ya kutuliza akili yake.
Mbangu ni mmoja wa watoto watatu waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela pamoja na baba yao Nguza.
Hata hivyo, Mbangu na Francis waliachiwa huru na Mahakama ya Rufani baada ya kushinda rufani yao wakati Nguza na mwanaye mwingine, Papii walirudishwa jela kuendelea na hukumu hiyo.
“Muziki upo kwenye damu yangu, siwezi kuuacha kabisa, lakini kwa sasa nimeamua kupumzika kwa mwaka wote wa 2010 ili nitulize akili yangu,”alisema.
Kabla ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, Mbangu alikuwa mwanamuziki wa bendi ya FM Academia akiwa anapiga drums.
Mbangu hakuwa tayari kuelezea maisha ya jela kwa kile alichodai kuwa, hapendi kukumbusha machungu, ambayo kwa sasa ameshaanza kuyasahau.
“Naepuka kukumbuka nilikopita, naepuka kujikumbusha majonzi,”alisema mwanamuziki huyo.
Mbangu alikiri kuwa, mara baada ya kutoka jela, alikuta mchumba wake ameolewa na mtu mwingine, hivyo hakuhangaika kumtafuta kwa sababu asingeweza kuvumilia kuwa mpweke.
“Nilikuwa na mchumba wangu, tulikuwa mbioni kufunga ndoa, lakini nilipotoka jela nikakuta ameshaolewa na mtu mwingine. Kwa sasa bado natazama nini la kufanya, sipendi kudandiadandia wanawake, huenda nikapata wangu,”alisema.
Mbangu alisema tangu alipotoka jela,amekuta mabadiliko makubwa kimuziki nchini, ambapo muziki wa Tanzania kwa sasa upo kwenye kiwango cha juu.
Alisema muziki wa sasa wa Tanzania hauna tofauti na ule wan chi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, isipokuwa hautangazwi sana kimataifa.

No comments:

Post a Comment