KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 13, 2011

Mnyama aitafuna Yanga

RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akikabidhi kombe la ubingwa wa Michuano ya Mapinduzi kwa nahodha wa Simba, Nico Nyagawa baada ya timu hiyo kuwachapa watani wao wa jadi Yanga mabao 2-0 katika mechi ya fainali, iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. (Picha na Bashir Nkoromo-picha zingine uk.4)

Na Abood Mahmoud, Zanzibar

SIMBA jana ilitwaa kwa mara ya pili ubingwa wa michuano ya soka ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuwachapa watani wao wa jadi Yanga mabao 2-0 katika mechi ya fainali, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Mabao yaliyoiwezesha Simba kutoka uwanjani kifua mbele yalifungwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Shija Mkina, moja katika kila kipindi, ikiwa ni mara ya pili kulinyakua kombe hilo baada ya mwaka 2008.
Mechi hiyo iliyoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki, akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ilikuwa ya kusherehekea miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Simba na Yanga kumenyana kwenye uwanja huo katika kipindi cha miaka 19 iliyopita. Kwa mara ya mwisho zilikutana mwaka 1992 katika mechi ya fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, ambapo Simba ilishinda kwa penalti 5-4.
Ushindi huo ulikuwa wa kulipiza kisasi kwa Simba, kufuatia kuchapwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa Oktoba 16 mwaka jana mjini Mwanza.
Kwa ushindi huo, Simba ilizawadiwa kitita cha sh. milioni tano wakati Yanga ilizawadiwa sh. milioni tatu. Timu zingine zilizoshiriki michuano hiyo ni Mtibwa Sugar, Azam, Zanzibar Ocean View, KMKM na Jamhuri.
Katika mechi hiyo, timu zote mbili zilicheza bila ya wachezaji wake kadhaa nyota waliopo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kinachoshiriki michuano ya Kombe la Nile, inayoendelea nchini Misri.
Simba iliwakosa kipa Juma Kaseja, mabeki Juma Nyoso na Kelvin Yondani pamoja na mshambuliaji Jabir Azizi wakati Yanga iliwakosa mabeki Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir Haroub na kiungo Nurdin Bakari.
Pamoja na kuibuka na ushindi, timu zote mbili hazikucheza soka ya kuvutia na kufanya mashambulizi ya kupanga. Kila timu ilicheza mpira wa kubutua na pasi za kubahatisha.
Simba ingeweza kupata bao dakika ya 13 wakati Patrick Ochan alipopewa pasi na Mussa Hassan ‘Mgosi’ akiwa ndani ya mita 18, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Yaw Berko wa Yanga.
Mgosi alipoteza nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao dakika ya 35 baada ya kushindwa kuunganisha krosi ya beki Haruna Shamte, aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.
Mshambuliaji huyo aliyetemwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars alisahihisha makosa yake dakika ya 33 baada ya kuifungia Simba bao, kufuatia pasi maridhawa ya Ochan.
Kiungo Omega Seme aliyeingia dakika za mwisho za kipindi cha kwanza badala ya Razak Halfan nusura aifungie bao Yanga dakika ya 44 alipopiga mpira wa adhabu ndogo umbali wa mita 20, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Batrhez’. Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Shija Mkina, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Hillary Echessa. Alifunga bao hilo baada ya kutanguliziwa pasi ndefu na Ochan.
Katika mechi hiyo, mwamuzi Ramadhani Mbega Kibo aliwaonyesha kadi za njano Ernesta Boakye, Juma Sefu na Salum Telela wa Yanga pamoja na Meshack Abel, Mohamed Banka na Haruna Shamte wa Simba.
Simba: Ally Mustapha, Haruna Shamte, Amir Maftah, Meshack Abel, Jerry Santo, Abdulrahim Humud, Mohamed Banka/Mbwana Samatta, Hillary Echessa/Shija Mkina, Mussa Hassan/Azizi Gila, Patrick Ochan na Nico Nyagawa.
Yanga: Yaw Berko, Salum Telela, Abuu Ubwa, Issack Boakye, Job Ibrahim, Ernest Boakye, Geofrey Bonny/Nsa Job, Juma Sefu/ Kigi Makasi, Razak Khalfan/Omega Seme, Idi Mbaga, Davis Mwape.

No comments:

Post a Comment