KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 13, 2011

Mgogoro wa ZFA utaikosesha Zanzibar uanachama wa FIFA

MGOGORO wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) wiki hii uliingia kwenye sura mpya baada ya kamati ya utendaji ya chama hicho kusema haiitambui kamati ya uchaguzi.
Kamati ya Utendaji ya ZFA ilitangaza kutoitambua kamati hiyo kwa madai kuwa, kuwepo kwake madarakani ni batili kwa sababu haikupewa baraka na chama hicho.
Uamuzi wa ZFA kutoitambua kamati hiyo ulikuja siku chache baada ya kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi mkuu wa chama hicho, kufuatia baadhi ya wagombea kuwa na kasoro.
Baadhi ya kasoro hizo ni pamoja na madai kuwa, mgombea wa urais, Ali Ferej Tamin hakuwa na sifa kutokana na kushindwa kuwasilisha cheti cha elimu yake ya kidato cha nne. Ferej ndiye aliyeshinda wadhifa huo baada ya kuwabwaga wagombea wenzake watatu.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Ali Suleiman Ali, maarufu kwa jina la Shihata alisema, kamati ya utendaji ya ZFA haina uwezo wa kutoitambua ama kuifuta kamati yake.
Shihata alisema, ili kamati hiyo ya utendaji ya ZFA isiitambue kamati yake, inapaswa kuwa na uongozi uliokamilika, akiwemo rais na makamu wawili wa rais kutoka Unguja na Pemba.
Kufuatia kuzuka kwa mgogoro huo, kamati ya uchaguzi imewateua Kombo Juma Hassan kuwa rais wa muda wa ZFA wakati Fadhil Ramadhani na Khamis Ameir Juma wameteuliwa kuwa makamu wawili wa rais kutoka Pemba na Unguja.
Pamoja na kuteuliwa kwa viongozi hao wa muda, Katibu Mtendaji wa ZFA, Mzee Zam Ali amesisitiza kuwa, uamuzi waliouchukua dhidi ya kamati ya uchaguzi ni sahihi na utabaki palepale.
Kwa mtazamo wangu, kilichojidhihirisha katika mzozo huu ni kutokuelewana kwa baadhi ya viongozi wa ZFA waliomaliza muda wao na wale wa kamati ya uchaguzi kutokana na baadhi yao kuweka mbele zaidi maslahi yao.
Hii ni kwa sababu haieleweki kwa nini ZFA iliwaruhusu wajumbe kutoka vyama shirikishi vilivyo chini yake kushiriki kwenye uchaguzi huo wakati uwepo wao madarakani ulikuwa batili.
Kadhalika haieleweki ni kwa nini kamati ya uchaguzi ilimruhusu Ferej ashiriki kwenye uchaguzi huo iwapo ni kweli kwamba hakuwasilisha cheti chake cha elimu ya sekondari kama taratibu zinavyotaka.
Uamuzi wa ZFA kutoitambua kamati ya uchaguzi pia ni wa kichekesho kwa sababu inakuwaje wanafikia uamuzi huo baada ya kamati hiyo kufuta matokeo ya uchaguzi na kutaka urudiwe upya?
Kutokana na hali ilivyo, nadhani ni vyema kwa vyombo vinavyosimamia michezo visiwani Zanzibar kuingilia kati mgogoro huo ili suluhu iweze kupatikana na kuinusuru ZFA isisambaratike.
Uamuzi pekee unaoweza kukinusuru chama hicho ni kurudiwa kwa uchaguzi huo na kuhakikisha taratibu zote katika kuuendesha hadi kupatikana kwa viongozi wapya zinaheshimiwa.
Haipendezi kuona kuwa, katika kipindi hiki ambacho Zanzibar inapigana kufa na kupona ili kupata uanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), ZFA imekumbwa na mgogoro mkubwa na haieleweki nini hatma yake.
Ni vyema Baraza la Michezo la Zanzibar (BMTZ) na wizara husika, kuitisha kikao kati ya pande husika ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo na kuondosha uwezekano wa FIFA kupuuza maombi ya visiwa hivyo kupatiwa uanachama.

No comments:

Post a Comment