KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 15, 2011

Wachezaji Yanga kuwekwa kiti moto


UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kuwaweka kiti moto wachezaji kwa kuwahoji mmoja mmoja ili kubaini sababu za timu hiyo kufanya vibaya katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Habari kutoka ndani ya Yanga zilieleza juzi kuwa, kikao hicho kilipangwa kufanyika jana makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuwahoji wachezaji hao ulifikiwa baada ya kikao kizito kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo.
Awali, uongozi wa Yanga uliwahoji makocha wa timu hiyo kuhusu sababu za kuboronga kwa timu hiyo na jana ulipanga kuwahoji wachezaji.
Mmoja wa viongozi wa Yanga, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alidokeza kuwa, wamefikia uamuzi huo ili kuhakikisha kuwa, wanapata ushahidi wa kutosha kabla ya kuwachukulia hatua wahusika.
Kiongozi huyo alisema wana hakika baada ya kumaliza kuwahoji wachezaji, watapata kiini cha tatizo hilo na hivyo kuamua hatua za kuchukua.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kikao hicho pia kitawahusisha wazee wa klabu hiyo kwa lengo la kupata busara zao kabla ya kuwachukulia hatua watu watakaobainika kuihujumu Yanga.
“Hatuwezi kuwachukulia hatua makocha au wachezaji kabla ya kuwahoji wahusika. Tunachotaka ni kujiridhisha kwa kupata ushahidi wa kutosha,”alisema.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alithibitisha jana kufanyika kwa uchunguzi huo, ikiwa ni pamoja na kuwahoji wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi.
Katika hatua nyingine, Nchunga alisema jana kuwa, kamati ya utendaji ya Yanga inatarajiwa kukutana hivi karibuni kuwajadili wanachama waliofungua kesi mahakamani kuupinga uongozi uliopo madarakani.
Nchunga alisema tayari wameshapokea maelekezo kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya wanachama hao.
"Hatuwezi kuwaacha waendelee kutuharibia klabu yetu, tutakutana na viongozi wa matawi ili kuwajadili vinara wa wanachama hao na kutoa uamuzi mbele ya wanachama,”alisema.

No comments:

Post a Comment