KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

Mchezaji wa Coastal Union alazwa Bombo


MSHAMBULIAJI wa timu ya Coastal Union, Shafii Kaluani(pichani) amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Tanga ya Bombo kufuatia mguu wake wa kulia kuvunjika mara mbili.
Mshambuliaji huyo machachari alivunjika mguu wakati wa mchezo baina ya timu hiyo na Ruvu Shooting uliofanyika wiki mbili zilizopita kwenye uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika hospitali ya Bombo na kumkuta mchezaji huyo akiwa amelazwa kwenye wodi ya majeruhi ya Galanos akiuguza mguu wake.
“Nina maumivu makali sana hapa nilipo, sijui hatma yangu itakuwaje,”alisema mchezaji huyo, ambaye amefungwa plasta ngumu mguuni (POP).
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Hafidh Badru alisema Kaluani alivunjwa mguu na beki mmoja wa Ruvu Shooting wakati walipokuwa wakigombea mpira.
Badru alisema wakati Kaluani alipokuwa akitolewa uwanjani, hawakuweza kutambua iwapo alivunjika mguu, lakini hali ilipozidi kuwa mbaya, ilibidi wamsafirishe haraka kumpeleka Bombo.
Alisema kuumia kwa mchezaji huyo kumeongeza pengo la wachezaji kwenye kikosi chake, ambapo idadi yao imefikia watatu wakati mchezaji mwingine mmoja anajiandaa kwa mitihani ya kidato cha nne.
Aliwataja majeruhi wengine kwenye kikosi chake kuwa ni Salum Juma na Benard Mwalala wakati Daniel Lianga amekwenda kwao Moshi kujiandaa kwa mitihani ya kidato cha nne.

No comments:

Post a Comment