KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

REDONDO: Moto wa Azam hauzimiki



KIUNGO Ramadhani Chombo ‘Redondo’ wa timu ya soka ya Azam, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwahakikishia ushindi katika mechi zijazo za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Redondo alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, ushindi walioupata dhidi ya Yanga ni salamu tosha kwa timu zingine watakazocheza nazo katika ligi hiyo.
Azam iliichapa Yanga bao 1-0 katika mechi iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na kuchupa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi sita, sawa na Mtibwa Sugar.
Azam ilitarajiwa kushuka tena dimbani jana kumenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Redondo aliieleza tovuti ya klabu hiyo kuwa, wamefanya maandalizi ya kutosha kupambana na timu yoyote watakayokutana nayo kwenye ligi hiyo.
“Timu ina hari nzuri na ari kubwa, kwa kuwa tumekuwa pamoja muda mrefu, tunahitaji ushindi kwa kila mechi tutakayocheza ili kufikia malengo yetu,” alisema.
Kiungo huyo wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars alisema, wanapigana kadri wawezavyo ili waweze kuchupa nafasi za juu zaidi katika msimamo wa ligi hiyo.
Nahodha msaidizi wa timu hiyo, Aggrey Morris alisema baada ya kutoka sare na Simba na kuichapa Yanga bao 1-0, hawaoni ni timu ipi inayoweza kuwazuia.
Amewataka wapenzi wa Azam wasiwe na wasiwasi kwa sababu wachezaji wote wapo makini, hivyo wajitokeze kwa wingi kwa sababu hawatawaangusha.

No comments:

Post a Comment