KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

Kanakamfumu aikosoa ligi kuu



Adai kuna matatizo kibao ya kiuendeshaji

Awaponda baadhi ya maproo kutoka nje

Asema Polisi Dodoma haijamtimua

SWALI: Umepokeaje taarifa za kuondolewa kwako katika kazi ya ukocha wa timu ya Polisi Tanzania?
JIBU: Binafsi nilikuwa nina mkataba wa muda mfupi na viongozi wa Polisi na mkataba huo umeshamalizika na tayari nimerudi katika shughuli zangu za kawaida.
Kwa ujumla, nimeondoka pale bila matatizo yoyote na hivi sasa ninaendelea na kazi yangu ya kufundisha soka sehemu nyingine.
SWALI: Ni sababu gani iliyoufanya uongozi wa Polisi Dodoma kutangaza kuwa umekuondoa? Na je, umejifunza nini katika kipindi chote ulichokuwa ukiinoa Polisi?
JIBU: Kama nilivyoeleza awali, nimeondoka Polisi baada ya mkataba wangu wa muda mfupi kumalizika na sipendi kuzungumza zaidi juu ya jambo hilo.
Lakini kama wao wanadai wameniondoa baada ya kugundua mwenendo wa timu hiyo sio mzuri, sawa lakini hiyo ni juu yao.
Kuhusu vitu, ambavyo nimejifunza kwa kweli ni vingi, kuanzia ndani ya ligi kuu na kwenye klabu hiyo. Sio siri, hivi sasa timu nyingi za ligi kuu zimejiandaa vizuri na kuifanya iwe na ushindani mkali wa kusaka ubingwa.
Maandalizi yamefanywa vizuri na kila timu na usajili umekuwa wa makini sana. Baadhi ya timu zimeweza kuibua vipaji, ambavyo vimeanza kutisha katika ligi hiyo.
Binafsi niliweza kusajili baadhi ya wachezaji chipukizi, ambao wameonyesha uwezo mkubwa na hivi sasa ni wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza.
SWALI: Ni mapungufu yepi uliyoweza kuyabaini katika ligi hiyo?
JIBU: Mapungufu ni mengi na makubwa kwa vile zipo baadhi ya timu zinategemea zaidi udhamini wa Vodacom, ambao bado ni mdogo ikilinganishwa na hali halisi ya michuano hiyo.
Timu zinapewa sh. milioni karibu 26 kwa mwaka, lakini maandalizi ya ligi hiyo yanaweza kuigharimu timu zaidi ya sh. milioni 200.
Bado kuna mapungufu mengine yakiwemo vifaa vya kufanyia mazoezi, uwezeshaji kwa wachezaji na vifaa duni, ambavyo ukiangalia, wachezaji mara nyingi kabla ya kumalizika ligi, viatu vyao navyo vinakuwa vimekwisha, inabidi wanunue vingine.
Hiyo yote inatokana na kuwepo vifaa visivyo na kiwango na kusababisha baadhi ya wachezaji kushindwa kuonyesha uwezo wao kutokana na kuvaa viatu vibovu.
SWALI: Vipi kuhusu uwezo wa waamuzi wa ligi kuu?
JIBU: Baadhi yao wanazingatia vyema sheria 17 za soka, lakiniwengine wanashindwa na kusababisha matatizo, ikiwemo kutaka kupigwa na wengine kuzinufaisha baadhi ya timu, hasa zenye uwezo kifedha.
Lakini kwa ujumla, inabidi TFF iangalie mwenendo wa baadhi ya waamuzi kwa vile wanakiuka miiko ya kazi hiyo.
SWALI: Vipi kuhusu mchuano wa kusaka namba katika vikosi vya kwanza?
JIBU: Kwa kweli mchuano ni mkali sana na katika baadhi ya timu, makocha wana kazi kubwa kutokana na kusajili wachezaji wengi wazuri.
Napenda kuwapongeza wachezaji wengi, ambao wamekuwa wakijituma katika ligi hiyo ili waweze kupata nafasi ya kucheza kwenye vikosi vya kwanza.
Hili jambo ni zuri kwa vile litachangia kwa asilimia nyingi kupatikana kwa vipaji zaidi ili viweze kushindana na wageni. Kwa sasa makocha wana kazi kubwa ya kuhitaji muda kuangalia uwezo wa kila mchezaji ili kujenga timu ya kwanza tofauti na zamani.
Pia inabidi makocha wafanyekazi ya ziada kufuatilia mienendo ya wachezaji nje ya dimba ili kuhakikisha wanafuata miiko ya soka.Mchezaji akimaliza mazoezi, inabidi atulie na wala asijihusishe na starehe, ikiwemo ya ngono kwa vile inaua uwezo wa mchezaji.
SWALI: Unawazungumziaje wanasoka wa kulipwa kutoka nje waliopo nchini?
JIBU: Kwa kweli wana mchango mdogo sana katika soka ya Tanzania tofauti na ule wa wachezaji wazawa, ambao wamekuwa wakionyesha uwezo mkubwa kuliko wao.
Hii yote inatokana na viongozi wa kamati za usajili, kusajili wachezaji kwa kuangalia majina au umaarufu wa nchi wanazotoka wachezaji hao. Hili jambo kwa kweli linaua uwezo wa timu kwa vile wanasajili wachezaji wenye uwezo mdogo.
Ukiangalia kwenye ligi kuu msimu huu, wapo baadhi ya wachezaji wazuri kutoka nje kama vile Yaw Berko, Haruna Niyonzima, Jerry Santo na Patrick Mafisango, ambao wanaonyesha uwezo mkubwa.
Lakini wengine kwa kweli wana uwezo mdogo,ingawa napenda kueleza kwamba, mchango wa wachezaji wa nje ni mzuri kwa vile utaweza kuwashtua wachezaji wetu.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu kuwepo mabadiliko ya viwanja kila kukicha kwa baadhi ya timu?
JIBU: Nilichogundua ni kwamba, kuna athari kubwa kwa vile timu nyingi zimekuwa zikilalamika kuingia gharama kubwa na wakati mwingine wachezaji kuchanganyikiwa.
Licha ya jambo hilo, baadhi ya wachezaji wanashindwa kuonyesha uwezo wao kutokana na kuhamishiwa katika viwanja vibovu.
Naliomba Shirikisho la Soka nchini (TFF), kubadili mfumo wa ligi kuchezwa katikati ya wiki kwa vile unawachosha sana wachezaji.
Angalia mchezaji mwishoni mwa wiki anacheza Dar es Salaam, na katikati ya wiki anatakiwa akacheze Bukoba katika mchezo mwingine.Ni vyema TFF ikalitazama jambo hilo kwa umakini mkubwa ili kupunguza athari na uwezo wa wachezaji.

No comments:

Post a Comment