KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 15, 2011

Kamati ya Tibaigana kukutana Sept 24

Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana tena Septemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza mashauri matatu dhidi ya Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu.
Awali kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana ilikuwa ikutane Agosti 29 mwaka huu kusikiliza malalamiko ya TFF dhidi ya viongozi hao, lakini kikao kiliahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake.
Pia TFF imewasilisha kwa kamati hiyo shauri jipya dhidi ya Sendeu kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Sendeu alimshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao, na anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba na kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima haikuwa halali.

SIMBA, POLISI ZAINGIZA MIL 16/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Polisi Dodoma iliyochezwa Septemba 14 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 16,839,000.
Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,257 ambapo kiingilio kilikuwa sh, 7,000 kwa mzunguko na sh. 20,000 kwa VIP.
Waliokata tiketi za sh. 20,000 walikuwa 80. Baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 2,568,661.02 kila timu ilipata sh. 3,546,671.90. Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 1,162,893.90), TFF (sh. 1,162,893.90), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 581,446.95), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 465,157.56) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 116,289.39).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment