KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 15, 2011

Simba kama Man United



SIMBA jana iliendelea kung’ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Polisi Dodoma bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yaliiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi tano, ikifuatiwa na JKT Ruvu yenye pointi tisa.
Mshambuliaji Gervas Kago ndiye aliyeiwezesha Simba kutoka uwanjani na pointi zote tatu baada ya kuifungia bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya tatu.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya kifua kutoka kwa Felix Sunzu. Lilikuwa bao la kwanza kwa Sunzu tangu ligi hiyo ilipoanza mwezi uliopita.
Ushindi wa Simba unafanana na ule wa Manchester United ya England, ambayo haijapoteza mechi hata moja tangu ligi kuu ya nchi hiyo ilipoanza. Hadi sasa, Simba imeshinda mechi tano na kutoka sare moja.
Simba ilianza ligi kwa ushindi wa mabao 2-0 ilipovaana na JKT Oljoro, ilishinda bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, iliilaza Villa Squad bao 1-0 kabla ya kutoka suluhu na Azam.
Timu hizo zilianza mchezo huo kwa kasi na Simba ilionekana kupania zaidi kufunga mabao ya mapema baada ya washambuliaji wake Ulimbokwa Mwakingwe, Kago na Okwi kuitoka mara kadhaa ngome ya wapinzani wao, lakini mashuti yao yalitoka nje na mengine kuokolewa.
Mwakingwe nusura afunge bao dakika 20 baada ya kufumua shuti kali lililotoka pembeni kidogo mwa lango kabla ya kiungo Patrick Mafisango kupiga mkwaju mkali uliwababatiza mabeki wa Polisi Dodoma na baadaye kuokolewa.
Dakika 34, Polisi Dodoma walifanya shambulizi langoni mwa Simba baada ya winga Bantu Admini kupata pasi ya Ibrahim Masawe, lakini kipa Juma Kaseja aliokoa. Mafisango aliyecheza vyema nafasi ya kiungo, aliitoka ngome ya Polisi Dodoma dakika 37 na kufumua shuti lilitoka nje ya lango.
Hamadi Kambangwa alifanikiwa kumtoka beki Juma Nyoso wa Simba na kutoa pasi nzuri kwa Admini dakika ya 56, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango kabla ya Kago kupiga mkwaju uliotoka nje kidogo ya lango la Polisi dakika mbili baadaye.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Cholo/Selemani Kapombe, Juma Jabu, Juma Nyoso, Victor Costa, Patrick Mafisango, Ulimboka Mwakingwe/Uhuru Selemani, Jerry Santo, Felix Sunzu, Gervas Kago, Emmanuel Okwi.
Polisi: Agathon Mkwandiko, Salmin Kisikisi, Nassoro Mhagama, Frank Sindato, Elias Maftah, Ibrahim Masawe, Brighton Mponzi, Haruna Hassan, Kulwa Mfaume, Hamad Kambangwa, Bantu Admini.

No comments:

Post a Comment