KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

Vodacom Mwanza Chalenji mwezi ujao

Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom, Rukia Mtingwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mbio za baiskeli za Vodacom Mwanza Chalenji uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Katikati ni Mwenyekiti wa Chama cha Baiskeli mkoa wa Shinyanga, Elisha Eliasi na kulia ni Katibu wa chama hicho, Lukas Bupilipili.


KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania imetangaza kuandaa na kudhamini mashindano ya mbio za baiskeli ya Vodacom Mwanza Chalenji yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom, Rukia Mtingwa aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, mbio hizo zitakazogharimu sh. milioni 50, zitaanzia Shinyanga na kumalizikia Mwanza.
Rukia alisema mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na amewaomba waendesha baiskeli wa miji hiyo miwili kujitokeza kwa wingi. Alisema washindi katika kila kundi watapewa zawadi mbalimbali, ambazo zitatangazwa baadaye.
“Mashindano haya yameboreshwa kwa zawadi, ubora na viwango, tofauti na miaka ya nyuma. Mashindano ya mwaka huu yatahusisha mikoa miwili muhimu kwa mchezo wa baiskeli katika kanda ya ziwa, yani Shinyanga na Mwanza,”alisema.
Rukia alisema mashindano hayo yatafanyika Oktoba 22 mwaka huu na yatakuwa ya kilomita 196 kwa wanaume na kilometa 80 kwa wanawake. Alisema kwa upande wa walemavu, mbio hizo zitakuwa za kilometa 15 kwa wanaume na kilomita 10 kwa wanawake.
Kwa mujibu wa Rukia, mashindano hayo, ambayo yamekuwa yakiandaliwa na Vodacom kwa miaka mitano sasa, yamelenga kukuza mchezo huo ili Tanzania iweze kujulikana zaidi kimataifa.
Alisema kwa kuzingatia kuwa mwaka huu, Tanganyika inasherehekea kutimiza miaka 50 ya uhuru, Vodacom imepanga kutoa zawadi ya mshiriki mwenye umri wa kuanzia miaka 50, atakayemaliza wa kwanza katika kundi la washiriki 50 wa kwanza.
Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Baiskeli mkoa wa Shinyanga, Elisha Eliya alisema,ili kuleta mabadiliko na kuboresha zaidi mashindano hayo, mbioza mwaka huu zitaanzia mkoa wa Shinyanga na kumalizikia Mwanza.
Amewataka wanamichezo wote wanaoshiriki katika mashindano hayo, kuanza kujiandaa mapema ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vyao wenyewe vya mchezo huo ili waweze kuwa katika hali nzuri ya kiushindani zaidi.

No comments:

Post a Comment