KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 1, 2016

YANGA YAZIDI KUUFUKUZIA UBINGWA


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walizidi kujisafishia njia ya kutetea taji lao baada ya kuichapa Toto Africans mabao 2-1.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Toto Africans ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwabao 1-0.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inazo pointi 65 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 58 na Simba yenye pointi 57.

Iliwachukua Toto dakika 39 kufunga bao la kwanza, lililopachikwa wavuni na Williams Kimanzi, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Abdalla Seseme.

Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga iliongeza kasi ya mchezo huku ikihaha kutafuta bao la kusawazisha, lakini ilikumbana na kizingiti kigumu cha mabeki wa Toto.

Juhudi za Yanga kusawazisha zilizaa matunda dakika ya 50 baada ya Amis Tambwe kufunga bao kabla ya Juma Abdul kuongeza la pili dakika ya 78.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo wakati miamba ya soka nchini, Simba na Azam itakapomenyana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment