Bao pekee na la ushindi la Yanga katika mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji Amis Tambwe dakika ya 19 baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima.
Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa itakutana na ndugu zao wa Azam katika mechi ya kwanza ya robo fainali itakayochezwa Jumatano kwenye uwanja huo wakati Gor Mahia ya Kenya itapambana na KCCA ya Uganda kesho.
Gor Mahia ilitinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi yake ya mwisho ya kundi A jana kwa kuichapa Telecom ya Djibouti mabao 3-0.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall, amesema kikosi chake kina kila sababu ya kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame.
Azam imetinga robo fainali ya michuano hiyo baada ya kuongoza kundi B ikiwa na pointi tisa, ikifuatiwa na KCCA ya Uganda yenye pointi saba.
Akizungumza baada ya Azam kuicharaza Adama City ya Ethiopia mabao 5-0, Hall alisema kikosi chake kimefanya vema katika mechi zote za hatua ya makundi kutokana na maandalizi mazuri.
"Hatuna sababu ya kukosa ubingwa wa Kombe la Kagame mwaka huu,"alisema kocha huyo raia wa Uingereza.
No comments:
Post a Comment