KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 8, 2016

MWALIMU NYERERE ALIKATAA KUKUTANA NA MUHAMMAD ALI




BINGWA wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Mohammad Ali, akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa zamani wa Dar es Salaam.

ILIKUWA Jumamosi ya Februari 2, 1980, wakati bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa za uzani wa juu, Muhammad Ali, alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa zamani wa Dar es Salaam.

Ali alikuja nchini akiwa ametumwa na Rais wa Marekani wakati huo, Jimmy Carter, kuja kuishawishi Tanzania isusie Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1980, iliyofanyika Moscow, Urusi.

Marekani ilitaka kuzishawishi nchi kadhaa za kiafrika, kususia michezo hiyo kutokana na kitendo cha Urusi, kuivamia kijeshi nchi ya Afghanistan mwaka 1979.

Bondia huyo machachari, ambaye kabla ya kubadili dini mwaka 1964, alikuwa akijulikana kwa jina la Cassius Clay, pia alitumwa kuzishawishi nchi za Kenya, Nigeria, Liberia na Senegal zisusie michezo hiyo.

Hata hivyo, ziara hiyo ya Muhammad Ali iliishia kwenye uwanja huo wa ndege huku akipokewa na mashabiki lukuki wa mchezo huo, wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, marehemu Chadiel Mgonja.

Ali hakuweza kukutana na Mwalimu Nyerere. Aliishia kukaa kwenye Hoteli ya Kilimanjaro kwa siku tatu kabla ya kuamua kuendelea na safari yake katika nchi zingine.

Licha ya umaarufu wake katika mchezo wa ngumi za kulipwa na ushawishi mkubwa wa ubalozi wa Marekani, juhudi za bondia huyo kukutana ana kwa ana na Mwalimu Nyerere ziligonga mwamba.

Imeelezwa kuwa Mwalimu Nyerere alikasirika kupangiwa kukutana na Muhammad Ali kwa vile aliona bondia huyo hakuwa na sifa ya kidiplomasia ya kukutana naye.

Baada ya kukwama kukutana na Mwalimu Nyerere, Ali ambaye pia alikuwa maarufu kwa jina la The Greatest, aliendelea na ziara yake katika nchi zingine nne, lakini aligonga tena mwamba alipokwenda Nigeria, ambako Rais wa zamani wa nchi hiyo, Alhaj Shehu Shagari aligoma kukutana naye.

Marais pekee aliobahatika kukutana nao na kuwawasilishia salamu kutoka kwa Rais Carter wa Marekani ni Daniel arap Moi wa Kenya, Leopold Sedar Senghor wa Senegal na William Tolbert wa Liberia.

Akiwa Senegal, bondia huyo alielezwa kwamba nchi hiyo inaongozwa kwa sera ya kutochanganya mambo ya michezo na siasa. Alifanikiwa kwenye nchi mbili tu za Kenya na Liberia.

Hata hivyo, baadaye Liberia ilibadili msimamo baada ya Rais Tolbert kupinduliwa Aprili, 1980, kabla ya kuanza kwa michezo hiyo, ambapo kiongozi wa mapinduzi hayo, Samuel Doe aliipeleka timu Moscow, lakini akaiondoa baada ya sherehe za ufunguzi.

Ziara hiyo ya Muhammad Ali haikuwa na mafanikio sana kwa vile kama angefanikiwa kuishawishi Tanzania, nchi nyingine nyingi za Afrika zingeweza kubadili msimamo.

Timu ya Tanzania ilikwenda Moscow kushiriki katika michezo hiyo na kufanikiwa kurudi nyumbani ikiwa na medali mbili za shaba, zilizonyakuliwa na wanariadha Filbert Bayi na Suleiman Nyambui.

Hiyo ndio michezo pekee ya Olimpiki, ambayo Tanzania iliambulia
medali. Bila shaka kama nchi nyingine zisingegoma, isingekuwa rahisi kwa Tanzania kupata medali hata moja.

Je, ni kwa nini Mwalimu Nyerere aliamua kuwakomalia Wamarekani kwa kukataa kugomea michezo hiyo?

Sababu hasa ni tukio la mwaka 1976, wakati wa Michezo ya Olimpiki iliyofanyika mjini Montreal, Canada.

Nchi za kiafrika zikiongozwa na Tanzania, mwaka huo, zilisusia michezo hiyo kutokana na kitendo cha timu ya New Zealand kuruhusiwa kushiriki.

Nchi za Afrika zikiongozwa na Tanzania, ziliiomba Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), isiiruhusu New Zealand kushiriki michezo hiyo kutokana na timu yake ya rugby, mwanzoni mwa mwaka 1976, kuzuru Afrika Kusini na kucheza na timu ya Afrika ya Kusini.

Kitendo hicho kilionekana ni kinyume na maazimio ya kuitenga Afrika ya Kusini kijamii na kiuchumi, kutokana na sera za ubaguzi wa rangi (apartheid).

Kutokana na ombi hilo kukataliwa, nchi nyingi za Afrika zilisusia michezo hiyo mwaka huo. Nchi nyingine kama Marekani, ziliendelea kushiriki bila kuziunga mkono nchi hizo za Afrika bila kujua ambacho kitatokea baada ya miaka minne.

No comments:

Post a Comment