KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 20, 2012

MTIBWA YATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA UHAI




Mtibwa Sugar imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu) kuzamisha African Lyon mabao 3-1.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, hadi mapumziko Mtibwa Sugar ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 22 na Hillary Kasela. Hassan Kabunda aliisawazishia African Lyon katika dakika ya 53.

Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Godfrey Mohamed dakika ya 64 na Juma Lazio akapachika la mwisho dakika ya 87.

Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar sasa itacheza mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Azam ambayo nayo leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu) iliilaza JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Chamazi. Bao la Azam lilifungwa dakika ya 46 na Mudathiri Yahya.

Mechi hiyo ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Nusu fainali ya pili nayo itachezwa kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10 kamili jioni.

Robo fainali ya tatu kati ya Oljoro JKT na Simba, na robo fainali ya nne zinachezwa leo saa 10 kamili jioni (Desemba 19 mwaka huu) kwenye viwanja vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment