'
Saturday, December 22, 2012
TAIFA STARS YAIGALAGAZA CHIPOLOPOLO, NGASA AWAPA RAHA MASHABIKI, SURE BOY 'MAN OF THE MATCH'
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jioni hii imewachapa mabingwa wa Afrika, Zambia bao 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Taifa Stars katika mechi hiyo alikuwa mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyefunga bao hilo la pekee na la ushindi katika kipindi cha kwanza.
Ngasa alifunga bao hilo kwa shuti kali akiwa pembeni ya uwanja, ambalo liligonga mwamba wa juu wa goli na kutinga wavuni.
Katika mechi hiyo, mchezaji aliyeng'ara kwa upande wa Taifa Stars alikuwa kiungo Salum Abubakar 'Sure Boy', ambaye aliumiliki vyema mpira na kucheza atakavyo, hali iliyosababisha wakati mwingine Wazambia waogope kumfuata kwa hofu ya kuaibika.
Mbali na Sure Boy, kiungo mwingine Frank Domayo naye alicheza vyema nafasi ya kiungo mshambuliaji, akishirikiana vyema na Mwinyi Kazimoto na Ngasa, ambao walikuwa mwiba kwa mabeki wa Zambia.
Amri Kiemba alilazimika kucheza mechi hiyo akiwa majeruhi, lakini aliweza kuelewana vyema na wenzake japokuwa hakuwa na kasi iliyozoeleka. Taifa Stars ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Zambia ilikianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji watano kwa mpigo kabla ya kuongeza wengine wawili kadri dakika zilivyokuwa zikiyoyoma. Walipotaka kuingiza wachezaji wengine wawili, mwamuzi Kirwa kutoka Kenya aliwakatalia.
Katika kipindi hicho cha pili, Taifa Stars ilimpumzisha Khamis Mcha na kumwingiza Simon Msuva kabla ya baadaye kuwatoa Ngasa na beki Kevin Yondan na kuwaingiza Amir Maftah na Nadir Haroub Cannavaro.
Wakizungumza na blogu ya liwazozito wakati wa mchezo huo, baadhi ya mashabiki walimpongeza kocha Kim Poulsen kwa uamuzi wake wa kuwachezesha wachezaji vijana wengi na wasiokuwa na majina.
Mshambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ambao wamekuwa wakidengua kuja kuichezea Taifa Stars, walijikuta wakiwa kwenye wakati mgumu baada ya kuzomewa na mashabiki.
Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Salum Abubakar, Amri Kiemba, Frank Domayo, Mrisho Ngasa/Amir Maftah, Mwinyi Kazimoto, Khamis Mcha/ Simon Msuva.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment