'
Monday, December 24, 2012
TFF YAIPONGEZA TAREFA, YATOA POLE KIFO CHA MUSA RICO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 22 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Tabora.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAREFA chini ya uenyekiti wa Yusuf Kitumbo aliyeshinda kwa kura 16 dhidi ya nane za Musa Ntimizi, na Paul Werema ambaye hakupata kura.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Tabora kwa kuzingatia katiba ya TAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti), Fate Remtulla (Katibu), Dick Mlimuka (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Razak Irumba (Mwakilishi wa Klabu TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Eric Kabepele na Mwalimu Sizya.
Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Coastal Union, Musa Rico kilichotokea jana (Desemba 22 mwaka huu) jijini Tanga.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti akiwa mchezaji Rico, na baadaye kocha alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Coastal Union, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Rico, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Desemba 23 mwaka huu) mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Rico mahali pema peponi. Amina
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment