KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 13, 2012

WACHEZAJI 20 WA U-20 KAGERA SUGAR WAPATA AJALI


TIMU ya vijana chini ya miaka 20 (U20) ya Kagera Suger waliokuwa wakitokea mkoani Kagera kuelekea jijini Dar es salaam kushiriki michuano ya Uhai CUP, wamenusurika kufa baada ya basi walilokuwa wakisafiria mali ya kampuni ya Super Najimunisa, kuligonga lori lililokuwa limeegeshwa kando kando ya barabara kuu ya Morogoro-Dodoma, ambapo utingo wa lori amepoteza maisha huku hali ya kocha wa timu hiyo ikiwa mbaya.
Mratibu wa Timu hiyo Mohames Hussein,akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi,alisema kuwa timu hiyo ilikuwa na wachezaji 14 na viongozi wawili, akiwemo kocha wa timu hiyo Ramadhan Feruz, ambaye alijeruhiwa katika ajali hiyo na hali yake ni mbaya,na alilazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu huku hali yake ikiwa ni mbaya na baadae aliandikiwa rufaa kwenda hospitali yaTaifa ya Muhimbili kwaajili ya matibabu zaidi.
Mchezaji wa timu hiyo, Ramadhan Yusuph alijeruhiwa na alitibiwa katika hospitali hiyo ya Rufaa na kuruhusiwa, huku yeye na wachezaji wenzake na kiongozi mwingine wa timu hiyo, wakitafutiwa basi jingine dogo kutoka kwa ndugu zao wa Mtibwa Sugar,kuendelea na safari ya Dar es salaam.
Kiongozi huyo wa Kagera alisema timu hiyo iliondoka Kagera tangu Desemba 09 mwaka huu, kushiriki michuano hiyo, lakini waliharibiwa na basi la Sumry wakitokea Kagera, ambapo walitafutiwa usafiri mwingine, ambao hata hivyo uliwaharibikia tena njiani na kupakizwa ndani ya Super Najimunisa ambalo nalo lilipata ajali na kusababisha kifo na majeruhi.
Kutokana na kocha wa timu hiyo kuumia, Kiongozi huyo wa Kagera alisema wamemtuma Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mlali Kabange, kwenda jijini Dar es salaam kuongoza timu hiyo ya vijana, huku wakiendelea na matibabu ya kocha huyo, ambaye akipata nafuu, atalazimika kurudishwa Kagera kwaajili ya mapumziko.
Mratibu huyo alisema kuwa wachezaji sita wa timu hiyo walishatangulia jijini Dar es salaam kwa ajili ya mashindano hayo ya UHAI CUP.
Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Morogoro RTO, Leonard Gyindo alisema ajali hiyo ilitokea Desemba 11 mwaka huu, majira ya saa moja jioni katika eneo la Dakawa,barabara kuu ya Morogoro-Dodoma, na kuhusisha basi la Super Najimunisa lenye namba T 186 AFY aina ya Scania ambalo liligonga lori lenye namba T229 ABA likiwa na tella namba 588 ASF mali ya kampuni ya Azam lilokuwa likitokea Dodoma kuelekea Morogoro, ambalo lilikuwa limeegesha njiani baada ya kuharibika.
Gyindo alisema dereva wa basi hilo ambaye hakufahamika, alikimbia baada ya ajali, na chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori hilo kuegesha gari bila kuonesha viashiria vyovyote vya tahadhari wakati akilifanyia matengenezo huku dereva wa basi naye mwendo kasi ukimfanya kushindwa kuliona lori hilo.
Katika ajali hiyo, Utingo wa lori Patric Merician mkazi wa Dakawa Morogoro alipoteza maisha, huku watu saba akiwemo kocha na mchezaji huyo wakijeruhiwa na baadhi yao wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo ya Mkoa wa Morogoro.

No comments:

Post a Comment