'
Thursday, December 13, 2012
SIMBA YAPATA KOCHA MPYA KUTOKA UFARANSA
Hatimaye klabu ya Simba imethibitisha kuvunja mkataba na kocha wake Mserbia, Milovan Cicovic ambapo sasa wanatarajia kumtambulisha kocha mpya kutoka Ufaransa.
“Huyu kocha ana uzoefu mkubwa sana. Zaidi ya ukocha wa kufundisha timu kubwa, alianzia maisha kwenye Academy, amepitia Academy ya Ufaransa ambayo ni maarufu sana na ndiyo iliyowatoa kina Thierry Henry wakati huo,"amesema leo Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga.
"Mbali na timu kubwa, atatutengenezea mfumo mzuri wa kutengeneza timu yetu ya vijana, sasa hivi Tanzania tunashindana na timu mbili za mamilionea,” ameongeza.
Kamwaga amesema pia kuwa, kocha huyo atasaidia kukuza viwango vya wachezaji wa Simba na kwamba, timu ya taifa pia itafaidika kwa sababu Simba ndio tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania.
Kuhusu suala la kumuuza Mrisho Ngassa kwenda kucheza soka ya kulipwa Sudan, Kamwaga amesema: “Sisi tumeshakubaliana na Azam kwamba Ngassa akiuzwa basi tutagawana nusu kwa nusu, lakini cha msingi Ngassa hawezi kuchezea timu nyingine hapa Tanzania ambayo siyo Simba kwa sababu tuna mkataba naye unaoisha Mei mwaka huu."
"Ngassa bado ni mchezaji wetu na tunatarajia kwamba mwishoni mwa wiki hii atajiunga kwenye mazoezi na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na ligi kuu ya Tanzania na michuano ya kimataifa,”aliongeza.
“Wanasema yeye aliongea na hiyo timu ya Sudan na kukubaliana kulipwa dola za kimarekani elfu 70 kwa hiyo kama atataka kwenda Sudan atakwenda, kama hatokwenda sisi tutamtumia, lakini hatuwezi kumpandisha ndege au kumlazimisha, kama atakwenda tutampa ushirikiano kwa asilimia 100 na kama hatotaka kwenda pia tutampa ushirikiano kwa asilimia 100,″ alisisitiza Kamwaga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment