KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, December 17, 2012

TENGA AWASHUKURU WALIOPIGIA KURA MAREKEBISHO YA KATIBA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kupigia kura waraka wa marekebisho ya Katiba, kwani wametimiza wajibu wao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo, Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba ni jambo muhimu, lakini lazima yapate ridhaa ya wanaohusika ambao ni wajumbe.
“Nawasukuru wajumbe kwa kupitisha jambo hili. Nawashukuru wote, waliokubali na waliokataa. Ndivyo demokrasia ilivyo. Tulitaka waseme ndiyo au hapana, hivyo tulitarajia kupata majibu yoyote kati ya hayo mawili.
Marekebisho mengine yalikuwa ni maelekezo (directives) kutoka FIFA na CAF. Katiba yetu inasema tutatekeleza maagizo ya CAF na FIFA, lakini kwa misingi ya utawala bora tuliona ni lazima tupate ridhaa kutoka kwa wajumbe,” amesema.
Jumla ya wajumbe waliopiga kura kwa njia hiyo ya waraka ni 103 ambapo 70 waliunga mkono wakati waliokataa ni 33. Idadi hiyo ni asilimia 68 ya kura zote zilizopigwa, hivyo kupatikana theluthi mbili ya kura zilizopigwa ili kufanya marekebisho kikatiba.
Vipengele vilivyoingizwa katika marekebisho hayo ni ‘club licencing’ kama ilivyoagizwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF kama ilivyoshauriwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Vilevile Kamati ya Utendaji itakutana Desemba 23 mwaka huu kufanya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi, kutokana na kupitishwa kwa marekebisho hayo ambayo yanaunda Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF. Pia itachagua wajumbe wa Kamati ya Rufani ya TFF.
Mkutano Mkuu wa TFF ambapo pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi utafanyika Februari 23 na 24 mwakani. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wanatakiwa kupewa taarifa ya Mkutano Mkuu siku 60 kabla.

No comments:

Post a Comment