KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 13, 2012

ZANTEL KUDHAMINI MKUTANO MKUU WA TASWA



Mkurugenzi wa wateja wakubwa wa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel Ahmed Seif Mohamed (kushoto ) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh.6,040,000 kwa Mwenyekiti wa chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa) Juma Pinto, pembeni ya Mohamed ni Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano na Masoko wa Zantel Awaichi Mawala na Katibu Msaidizi wa Taswa, George John. (Na Mpigapicha Maalum).


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zantel imejitokeza kudhamini Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utakaofanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani Pwani.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Zantel Ahmed Seif Mohamed, alisema wanajisikia furaha kushirikiana na TASWA kudhamini mkutano huo wa aina yake.

Alisema Zantel imekuwa na uhusiano mzuri na wanahabari, hivyo walipoombwa hawakusita kufanya hivyo na wana matumaini makubwa utakuwa mkutano wenye manufaa.

Alieleza kuwa kampuni yake baada ya kupata mafanikio katika mashindano ya Epiq Bongo Star Search iliyomalizika hivi karibuni ni nafasi nyingine ya kuendelea kudhamini matukio mbalimbali ya michezo na burudani kwa kadri uwezo utakavyoruhusu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru Zantel na kusema awali chama hicho kiliomba udhamini kwa kampuni hiyo kwa lengo la kufanya mkutano Dar es Salaam, lakini sasa walifikiria ufanyike Bagamoyo, Pwani.

Alisema Zantel wamedhamini kwa kiasi cha Sh 6,040,000 na kwamba bajeti ya mkutano huo ni Sh milioni 20, hivyo kuomba wadau wengine wasaidie ili kufanikisha mkutano huo utakaohusisha zaidi ya waandishi wa habari za michezo 100 ambao ni wanachama wa TASWA.

“Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wanachama 100, na pia watakuwepo wadau mbalimbali wa TASWA wakiwemo waandishi wakongwe wa habari za michezo wambao watapewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo,” alisema Pinto.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho,Amir Mhando aliwasisitiza wanachama kuendelea kuthibitisha ushiriki wao na kuwa mwisho wa kufanya hivyo ni kesho alasiri.

No comments:

Post a Comment