'
Tuesday, December 11, 2012
YANGA YADAIWA KUMTEKA NYARA NGASA, SIMBA NA AZAM ZAKATA MZIZI WA FITINA
KLABU ya Yanga inadaiwa kumteka nyara na kumficha mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyesaliwa kwa mkopo na Simba akitokea Azam.
Wasiwasi wa Ngasa kufichwa na Yanga umekuja saa chache baada ya Simba na Azam kufikia makubaliano ya kumuuza mchezaji huyo wa klabu ya El-Merreikh ya Sudan.
Simba na Azam zimefikia makubaliano hayo leo mchana baada ya kikao cha pamoja kati yao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ngasa ameuzwa El-Merreikh kwa kitita cha dola za Marekani, 100,000, lakini baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, mchezaji huyo amekuwa hapatikani kwa simu yake ya mkononi.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema jana kuwa, viongozi wa El-Merreikh wamekuwa wakimtafuta Ngasa kwa njia ya simu tangu mchana, lakini hapatikani na haieleweki mahali alipo.
Rage alisema wana wasiwasi kuwa, mchezaji huyo huenda amefichwa na wapinzani wao wa jadi Yanga, baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba wanataka kumsajili.
Hata hivyo, Rage amesema Yanga hawana uwezo wa kumsajili Ngasa kwa sasa kwa vile mkataba wake na Simba unatarajiwa kumalizika Mei mwakani.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Bin Kleb alipoulizwa leo, amesema hawezi kusema lolote, isipokuwa atafutwe kuanzia kesho au keshokutwa.
Bin Kleb hakuwa tayari kukubali au kukataa kuhusu klabu yake kumficha Ngasa, zaidi ya kusisitiza kuwa atafutwe katika siku hizo mbili.
Kwa upande wake, Rage aliipongeza Azam kwa uamuzi wake wa kukubali kuketi meza moja na klabu yake kwa ajili ya kufikia uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya mchezaji huyo.
Viongozi wa klabu hizo mbili wamekubaliana kugawana dola 50,000 kila upande, ambazo zitalipwa na El-Merreikh kwa ajili ya kumnunua mshambuliaji huyo, ambaye alijiunga na Azam akitokea Yanga.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Ngassa atapokea kiasi cha $75,000 kama gharama ya usajili kwa mkataba wa miaka miwili, na pia atalipwa kiasi cha $ 4,000 kama mshahara kwa kila mwezi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment