'
Thursday, December 6, 2012
KILI STARS, ZANZIBAR HEROES KAZI IPO LEO
TIMU za soka za Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na Zanzibar, Zanzibar Heroes leo zitakuwa na vibarua vigumu wakati zitakaposhuka dimbani kumenyana na Kenya na Uganda katika mechi za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji.
Wakati Zanzibar Heroes itamenyana na Kenya katika mechi ya kwanza ya nusu fainali itakayopigwa kuanzia saa 10 jioni, Kilimanjaro Stars itakipiga na wenyeji Uganda katika mechi ya pili itakayoanza saa 12 jioni.
Mechi hizo mbili zina umuhimu mkubwa kwa Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes kwa vile iwapo zitashinda, zitaweka rekodi ya kukutana kwa mara ya kwanza katika fainali ya michuano hiyo.
Kilimanjaro Stars ilifuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuitoa Rwanda kwa mabao 2-0 katika mechi ya robo fainali iliyopigwa Jumatatu iliyopita wakati Zanzibar Heroes iliitoa Burundi kwa penalti 6-5 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.
Wenyeji Uganda wamefuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuitoa Ethiopia kwa mabao 2-0 katika mechi ya robo fainali iliyopigwa juzi wakati Kenya iliitoa Malawi kwa kipigo cha bao 1-0.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Heroes, Kim Poulsen alisema vijana wake wote wapo fiti na wana ari kubwa ya kuwatoa wenyeji katika hatua hiyo.
Kivutio kikubwa katika mechi hiyo kitakuwa kwa wachezaji Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza wa Uganda, ambao watakabiliana na ukuta mkali wa Kilimanjaro Stars utakaokuwa ukiongozwa na Shomari Kapombe na Kevin Yondan.
Okwi na Kapombe wanacheza pamoja katika klabu ya Simba wakati Kiiza na Yondan wanacheza pamoja katika klabu ya Yanga, hivyo wanajuana vyema.
Waganda hao wawili wamekiri kwamba, mechi hiyo itakuwa ngumu, lakini wameapa kucheza kufa na kupona kuhakikisha wanashinda na kufuzu kucheza fainali.
Safu ya kiungo ya Kilimanjaro Stars inatarajiwa kuongozwa na Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba, ambaye hucheza kama kiungo mshambuliaji. Pia watakuwemo John Boko na Mrisho Ngasa, ambao wanaoongoza kwa ufungaji mabao katika michuano hiyo.
“Inahitaji maarifa sana kuweza kupenya pale, Shomary (Kapombe) ni mchezaji mwenye akili sana na anajituma, Yondan (Kevin), pia ana akili sana, mzoefu na anajituma," alisema Okwi alipokuwa akizungumzia mechi hiyo jana.
"Mimi nimemkuta pale Simba hadi anahamia Yanga (msimu huu). Na tangu nakuja Simba, yeye ni mchezaji wa timu ya taifa, wana Kaseja (Juma) kipa mzuri na mzoefu, tena sana, kwa hivyo ukuta wao ni mzuri sana, ila na sisi tuna safu kali sana ya ushambuliaji, Diego (Hamisi Kiiza), Brian (Umony), Ssentongo (Robert), Kizito (Geoffrey) na mimi, wote nadhani unajua cheche zetu.Kwa hivyo hiyo mechi itakuwa sana,"aliongeza.
Hadi sasa, ukuta wa Uganda haujaruhusu bao hata moja wakati safu ya ulinzi ya Kilimanjaro Stars imeruhusu bao moja la Selemani Ndikumana wa Burundi katika mechi ya makundi.
Kwa upande wa Zanzibar Heroes, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Bausi amejigamba kuwa, wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa wanaibuka na ushindi dhidi ya Kenya.
Bausi alisema wameiona Kenya ikicheza katika mechi ya robo fainali dhidi ya Malawi na kuiita kuwa ni timu isiyotisha, inayofungika na ambao haiwezi kuwapa wakati mgumu.
Tegemeo kubwa la Zanzibar katika mechi hiyo litakuwa kwa mshambuliaji wake, Mcha Khamis, ambaye hadi sasa amefunga mabao mawili.
Wachezaji wengine wa Zanzibar Heroes wanaotarajiwa kuwa tegemeo kubwa katika mechi ya leo ni kipa Mwadini Ally, Aggrey Morris, Saleh Mohamedi, Jaku Juma na Samir Haji Nuhu.
Katika kujiimarisha kwa ajili ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Kenya, James Nandwa ameamua kuwarejesha kwenye kikosi chake wachezaji Paul Were na Kevin Omondi, ambao walitimuliwa wiki iliyopita kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Nandwa alikaririwa na gazeti la Daily Nation la Kenya jana akisema kuwa, ameamua kuwarejesha wachezaji hao baada ya kuomba radhi na kuamua kuwasamehe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment