KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 6, 2012

MSHINDI MISS EAST AFRICA KUZAWADIWA GARI NA DOLA 30,000



WAANDAAJI wa mashindano ya kumsaka mrembo wa Afrika Mashariki wametenga zawadi zenye thamani ya sh. milioni 100 kwa ajili ya washindi wa mwaka huu.
Mratibu wa mashindano hayo, Rena Callist aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, mshindi wa kwanza atazawadiwa dola 30,000 za Marekani pamoja na gari aina ya Mazda lenye thamani ya dola 15,000.
Mbali na zawadi hizo, Rena alisema mshindi huyo atapata mkataba wa kufanyakazi za Miss East Africa Organization wenye thamani ya dola 15,000.
Kwa mujibu wa Rena, mshindi wa pili atapata zawadi zenye thamani ya dola 8,000 na pesa taslim dola 2,000 na mkataba wa kufanyakazi na Miss East Africa Organization wenye thamani ya dola 6,000.
Alisema mshindi wa tatu atapata zawadi zenye thamani ya dola 5,000 na pesa taslim dola 1,500 na mkataba wa kufanyakazi na Miss East Africa Organization wenye thamani ya dola 3,500.
Mashindano hayo, ambayo awali yalipangwa kufanyika leo kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, sasa yamesogezwa mbele hadi Desemba 21 mwaka huu.
Alisema lengo la kusogeza mbele mashindano hayo ni kutoa fursa zaidi kwa washiriki kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini na kuvitangaza kupitia mashindano hayo.
Warembo wanaotarajiwa kushiriki katika shindano hilo wanatoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia na Djibouti.
Nchi zingine ni Eritrea, Sudan, Ethiopia, Malawi, Shelisheli, Sudan Kusini na warembo walioshinda mataji ya Afrika Mashariki katika nchi za Ubelgiji, Ufaransa na Uholanzi.
Shindano hilo limedhaminiwa na Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, TANAPA, Shirika la Ndege la Ethiopia, DTP, Ako Catering, Darlings Hair, Satguru na Clouds FM.

No comments:

Post a Comment