KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, December 29, 2012

KESI YA LULU YASAJILIWA RASMI MAHAKAMA KUU



JALADA la kesi ya kuua bila kukusudia la msanii nyota wa filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' tayari limetua Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kesi yake imesajiliwa.

Lulu anakabiliwa na mashtaka ya kumuua bila kukusudia, aliyekuwa msanii maarufu wa fani hiyo nchini, Steven Kanumba kinyume cha kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu.

Awali, kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali ukiwamo upeelelezi, huku akikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia kinyume cha kifungu cha 196.

Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia.

Desemba 21, 2012, Lulu alisomewa maelezo ya kesi, yakiwemo ya mashahidi watakaotoa ushahidi dhidi yake na maelezo yake aliyoyatoa polisi, kisha Mahakama ya Kisutu ilifunga rasmi kesi hiyo na kutamka rasmi kuihamishia Mahakama Kuu, ambako ndiko itakakosikilizwa.

Habari zilizopatikana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana zilisema kuwa, tayari kesi hiyo imeshapokelewa mahakamani hapo na kupewa usajili wa shauri la jinai namba 125 mwaka 2012.

Hata hivyo, habari hizo zilisema kuwa kwa sasa kesi hiyo inasubiri kupangiwa Jaji atakayeisikiliza baada ya taratibu zote za kimahakama kukamilika, kwa tarehe itakayopangwa na msajili kulingana na ratiba ya vikao vya mahakama hiyo.

Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, Aprili 7, 2012, nyumbani kwake Sinza Vatican, Dar es Salaam. Wakati akisoma maelekezo ya kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro alidai kuwa, upande wa mashtaka utawaita jumla ya mashahidi tisa.

Wakili Kimaro pia alidai kuwa, upande wa mashtaka utawasilisha mahakamani vielelezo kadhaa vitakavyotumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo, ikiwamo ramani ya eneo la tukio kwenye chumba alimofia Kanumba, ripoti ya uchunguzi wa kifo na maelezo ya onyo la Lulu.

Wakili Kimaro alidai kuwa, Aprili 7, 2012, Lulu alitoa maelezo ya onyo, kuhusiana na tuhuma zinazomkabili, katika kituo cha polisi cha Oysterbay, yaliyochukuliwa na askari wa kituo hicho, mpelelezi Sajenti Renatus.

Kwa mujibu wa maelezo hayo ya onyo, Lulu alizaliwa mwaka 1994 na alimaliza kidato cha nne katika shule ya sekondari Midway na kwamba baada ya hapo, aliendelea na shughuli za sanaa kuanzia mwaka 2000.

GAZETI LA MWANANCHI DES 29, 2012

No comments:

Post a Comment