'
Thursday, December 6, 2012
YANGA, AZAM ZAMTOSA OKWI
UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema hauna mpango wowote wa kutaka kumsajili mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kikosi chao kimekamilika kwa idadi ya wachezaji wa kigeni, hivyo hakuna nafasi ya Okwi.
Mwalusako ameelezea msimamo wake huo baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Yanga na Azam zimepania kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda wakati wa dirisha dogo Januari mwakani.
"Hatuna kabisa mpango wa kumsajili Okwi. Tayari kikosi chetu kinao wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni, hivyo hatuhitaji mchezaji mwingine wa kigeni,"alisema Mwalusako.
Mwalusako amesema wanashangazwa na taarifa, ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na baadhi ya vyombo vya habari kwamba, Yanga imemtengea mchezaji huyo zaidi ya sh. milioni 300.
"Hii si kweli hata kidogo. Hatuwezi kutenga kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya mchezaji mmoja. Ninachosisitiza ni kwamba hatumuhitaji Okwi na hana nafasi kwenye kikosi chetu,"alisema.
Kwa mujibu wa Mwalusako, wakati wa usajili wa dirisha dogo, wamepanga kusajili wachezaji wazalendo wachache kutoka katika klabu za ligi kuu.
Wachezaji wa kigeni waliopo sasa katika klabu ya Yanga ni Yaw Berko, Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu na Mbuyu Twite.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Azam umesema hauna mpango wa kumsajili Emmanuel Okwi wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Meneja wa Azam, Patrick Kahemele alisema jana kuwa, baadhi ya viongozi wa Azam wamekwenda Uganda kwa ajili ya kusaka nyota wengine wa kigeni na si Okwi.
Kahemele alisema klabu yake imepanga kusajili wachezaji watatu wapya wa nafasi za beki wa kati, kiungo na mshambuliaji.
Alisema tayari wameshafanikiwa kuwanasa kiungo kutoka Kenya na mshambuliaji kutoka Ivory Coast, lakini hakuwa tayari kutaja majina yao.
Alipoulizwa kuhusu wachezaji watakaoachwa, Kahemele alisema wanatarajia kuwatangaza baada ya kupata idhini kutoka kwa bodi ya wakurugenzi.
Kuna habari kuwa, Azam imeamua kumwacha moja kwa moja beki Said Mourad na kuwarejesha kundini Aggrey Morris na Deogratius Munishi 'Dida'.
Wachezaji hao watatu wamesimamishwa kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa timu pinzani wakati wa mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment