'
Wednesday, December 5, 2012
TENGA ANAHUJUMIWA?
BAADHI ya wapambe na wanamichezo wanaotaka kuwania uongozi wa juu katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameanza kuzunguka mikoani kwa ajili ya kufanya kampeni chafu za kupinga waraka wa kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo.
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, imeamua kusogeza mbele uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo ili kutoa nafasi kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano kutia saini marekebisho ya katiba.
Kipengele, ambacho kimezua balaa na kufanyiwa hujuma na baadhi ya wagombea hao kupitia kwa wapambe wao ni kile kinachohusu 'Club Licensing' kama ilivyoagizwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kupitia waraka wake kwa nchi wanachama.
Katika waraka huo, FIFA imezitaka nchi wanachama kuhakikisha kuwa, kipengele hicho kinaingizwa kwenye katiba za vyama vyao.
Kutokana na maelekezo hayo ya FIFA, TFF inatakiwa kuunda Kamati ya Rufani ya Uchaguzi (Elections Appeals Committee) na kuondokana na utaratibu wa sasa ambapo Kamati ya Rufani (Appeals Committee) imejigeuza kuwa kamati ya rufani ya uchaguzi wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Maelekezo mengine ya FIFA kwa nchi wanachama ni kuondolewa kwa nafasi ya makamu wa pili wa rais na kutamka kuwa, wawakilishi wa klabu za ligi kuu katika kamati ya utendaji watachaguliwa moja kwa moja na klabu zenyewe.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji,Alex Mgongolwa, baada ya kutafakari mapendekezo hayo, kamati ya utendaji ya TFF imeamua kuwa wajumbe wote wa mikoani wapelekewe waraka huo na kuusaini ili sheria hiyo ianze kutumika.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wanaotaka kuwania uongozi TFF, wanapinga maelekezo hayo kwa madai kuwa, hizo ni mbinu za viongozi wa shirikisho hilo kutaka wakae madarakani kwa muda mrefu zaidi.
Akizungumzia kampeni hizo chafu, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema jana kuwa, wanaopinga waraka huo hawana hoja kwa vile shirikisho hilo halina hila yoyote ya kutaka kuendelea kuwepo madarakani kwa vile muda wao umemalizika.
"Unajua wapo wanaoeneza habari hizo, lakini ukweli ni kwamba sisi hatuna hila, isipokuwa hali ya kifedha sio nzuri, hivyo kazi hiyo inabidi ifanywe na wajumbe huko huko walipo,"alisema.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, tayari wanaopinga marekebisho hayo wameshatembelea mikoa ya Kagera na Kigoma na kuwashinikiza viongozi wake wasiyakubali.
Katibu wa Chama cha Soka cha Kigoma, Issa Bukuku alikaririwa wiki hii akisema kuwa, hawawezi kutia saini waraka huo, badala yake wanasubiri kuitishwa kwa mkutano mkuu wa shirikisho hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment