KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, December 5, 2012

VENUS, SERENA WAMZIMIA D'BANJ



LAGOS, Nigeria
WACHEZA tennis nyota wa Marekani, Venus na Serena Williams, ambao walikuwepo nchini Nigeria kwa ziara maalumu, wameeleza kuvutiwa kwao na mwanamuziki D'Banj.
Venus na Serena walisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kujumuika na mashabiki kucheza wimbo wa D'Banj unaojulikana kwa jina la Oliver Twist.
Wacheza tennis hao walielezea mapenzi yao kwa mwanamuziki huyo kwenye uwanja wa tennis wa mjini Lagos, ambapo walishiriki kucheza mechi maalumu za mchezo huo.
Venus na Serena waliwashangaza mashabiki waliokuwa wamefurika kwenye uwanja huo baada ya kucheza kwa umahiri mkubwa kibao cha Oliver Twist na kuwafanya wawashangilie.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadaye kwenye hoteli ya Federal Palace mjini Lagos, wacheza tennis hao walisema wamekuwa mashabiki wa D'Banj kwa muda mrefu ndio sababu walipatwa na wazimu wakati DJ alipocheza kibao hicho uwanjani.
"D'Banj si mgeni kwetu. Ni shabiki wetu mkubwa na ni mmoja wanamuziki mahiri kutokea barani Afrika,"alikiri Venus.
"Pia tunaupenda sana muziki wake na tumesikitika kwa kutojumuika nasi leo. Lakini yote ni mamoja, tumefurahia ziara yetu,"aliongeza msanii huyo.
Kwa upande wake, Serena alisema: "Siku zote tumekuwa tukivutiwa naye na kumpenda. Tunaipenda staili yake ya muziki, ni alama ya muziki wa kiafrika."
Serena alisema wamejifunza mengi wakati wa ziara yao nchini Nigeria na kamwe hawakuwahi kupata wasaa mzuri kama huo katika kazi yao ya kucheza tennis.
"Tunaamini ziara yetu hii itafungua njia kwa vijana wa Nigeria, ambao wamekuwa wakivutiwa na mafanikio yetu. Ziara hii itabaki kwenye kumbukumbu katika maisha yetu yote,"alisema Serena huku akitabasamu.
Wacheza tennis hao walieleza kufurahishwa kwao na upendo ulioonyeshwa na vijana wa Nigeria wakati wote wa ziara yao, licha ya kuwepo nchini humo kwa kipindi kifupi.
"Hii ni ziara yetu ya kwanza Afrika na tumejisikia tupo nyumbani na kufurahia kila sekunde tuliyokuwepo hapa, kuanzia tulipowasili kwenye uwanja wa ndege. Tutafurahia kuja tena wakati mwingine,"alisema Venus.
Baada ya waandaaji wa ziara ya wacheza tennis hao kugundua kwamba, walikuwa na hamu kubwa ya kukutana ana kwa ana na D'Banj, walijaribu kuwasiliana na mwanamuziki huyo, lakini ilishindikana.

No comments:

Post a Comment