KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, December 3, 2012

KOCHA SERENGETI BOYS AJIPA MOYO, MADADI ASIMULIA UNYAMA WALIOFANYIWA NA CONGO BRAZAVILLE



Kocha wa timu ya taifa ya vijana, Jacob Michelsen amesema kuwa anajivunia vijana wake licha ya kuondolewa na Congo kwenye mashindano ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na kulaumu uamuzi kuwa ulichangia kwa kiasi kikubwa Serengeti Boys kulala kwa mabao 2-0 mjini Brazaville.
Kwa matokeo hayo, Serengeti Boys imeondolewa kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17 kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Dar es salaam kuisha kwa Tanzania kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa. Timu hiyo itarejea nchini siku ya Jumanne saa 1:00 jioni kwa ndege ya Kenya Airways.
“Vijana walicheza vizuri sana na walicheza kwa juhudi wakati wote wa mchezo na safari hii wacheza dhidi ya vijana ambao ni wakubwa zaidi,” alisema kocha huyo kutoka Denmark. “Lakini waliangushwa na uamuzi kwa sababu walipata penati ambayo haikustahili.
“Kwa kweli hata tukio lenyewe lilitokea nje ya penati na beki wetu alilala kuchukua mpira na alifanikiwa kuufikia bila ya kumgusa mshambuliaji wa Congo. Lakini wakati beki wetu akiwa ameshauchukua mpira na yule aliyejiangusha akiwa ameshanyanyuka, mwamuzi alipiga filimbi kuamuru penati.”
Kocha huyo alisema pamoja na bao hilo Serengeti Boys iliendelea kucheza vizuri na nusura mchezo huo uamuliwe kwa penati tano, lakini wenyeji wakapata bao la pili lililoinyima Tanzania nafasi ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali hizo.
“Lilikuwa ni bao lilitokana na shambulizi la kushtukiza na walikimbia vizuri na mpira na baadaye kupiga krosi iliyounganishwa kwa kichwa,” alisema Michelsen.
“Najivunia vijana wangu kwa sababu walicheza kwa kujituma na kujiamini; walifanya juhudi kubwa, lakini uamuzi ulituangusha. Nina imani na timu hii na natumaini kama vijana watano walitoka kwenye timu ya U-20 na kuingia timu ya taifa, basi kuna vijana wengine wanaoweza kutoka kwenye timu hii na kuingia timu ya taifa. Ni vizuri tukaendelea na programu za vijana tuweze kujenga timu nzuri baadaye.”
Afisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi ambaye aliambatana na timu hiyo Congo, alisema mechi hiyo ilizingirwa na mizengwe kabla na baada ya mechi na kwamba wamesharipoti matukio yote kwa kamisaa wa mechi hiyo baada ya kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo, mtunza vifaa Juma Kizwezwe na mkalimani wa timu kushambuliwa na polisi na mashabiki kabla ya mechi hiyo.
“Hatukupewa gari la polisi wakati wa kwenda uwanjani na hivyo hatukujua tuingilie wapi. Tulipofika uwanjani, walituelekeza mlango ambao tuliona wanaumwagia maji ambayo Julio aliona yangeathiri wachezaji na kuwaagiza wasitumie mlango huo na ndipo polisi walipomvamia,” alisema Madadi.
“Kizwezwe alishambuliwa na mashabiki baada ya kamisaa kumuagiza arejee hotelini kufuata jezi zaidi kutokana na Congo kuwasilisha pingamizi kabla ya mechi kuwa jezi za Tanzania hazikuwa kwenye mlolongo uliokuwa kwenye orodha iliyowasilishwa.
“Alipotaka kutoka uwanjani, alizuiwa na askari na tukalazimika kumuita kamisaa ambaye aliagiza polisi wamruhusu atoke uwanjani. Alipotoka mashabiki walimzuia asiondoke na mzozo ulipokuwa mkubwa mashabiki walimvamia na ndipo tulipomwita tena kamisaa ambaye aliagiza Kizwezwe asiondoke na badala yake jezi zilizokuwa na matatizo zibandikwe plasta. Hata hivyo, polisi walimzuia Kizwezwe asiende kukaa kwenye benchi hadi mchezo ulipoisha.”
Madadi alisema kuwa kutokana na vurugu hizo, kamisaa huyo kutoka Afrika Kusini aliomba majina ya walioshambuliwa na akaahidi kuyaweka matukio hayo kwenye ripoti yake.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema Shirikisho limeyapokea matokeo hayo kwa masikitiko kutokana na ukweli kwamba TFF ilifanya juhudi kubwa katika kuhakikisha safari hii timu za vijana zinapata maandalizi mazuri na ya muda mrefu, lakini juhudi hizo zimekwamishwa na mazingira mabaya kama yalivyoripotiwa na viongozi wa msafara wetu.
“Katika kutafuta mafanikio hakuna njia ya mkato. Ni lazima tuamini katika program tunazozitekeleza na kuboresha pale tunapoona pana udhaifu. Tunaamini kuwa itafika wakati juhudi hizi zitazaa matunda na Watanzania watanufaika na mipango hii ya muda mrefu,” alisema katibu huyo

No comments:

Post a Comment