KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, December 1, 2012

TFF YAICHONGEA TP MAZEMBE CAF



RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amefanya mazungumzo na Rais wa shirikisho la mchezo huo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuhusu washambuliaji wa timu ya taifa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.

Wachezaji hao wamezuiwa na klabu yao ya TP Mazembe wasirejee kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars ambayo inashiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea jijini Kampala, Uganda kwa madai kuwa klabu hiyo inajiandaa kwa mechi za kirafiki baadaye mwezi huu.

Tenga alifanya mazungumzo hayo na Omari Constatine, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) wakati wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Chalenji jijini Kampala.

Mbali na mazungumzo hayo, tayari Tenga ameshamwandikia barua rais huyo wa Congo akirejea mazungumzo baina yao juu ya kuwaruhusu washambuliaji hao nyota kujiunga na Kilimanjaro Stars ambayo imeshashinda mechi moja na kupoteza moja kwenye michuano ya Kombe la Chalenji.

“Kwa kuwa kanuni zinawezaz kuwa zinaitetea klabu, tunaomba msaaada wako na ufahamu wako wa masuala ya uongozi wa klabu ili tuweze kupata huduma za wachezaji hawa wawili kwa ajili ya mashindano haya muhimu kwa nchi yetu na CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati),” inasema sehemu ya barua hiyo ya Tenga.

Samata na Ulimwengu walitoa mchango mkubwa kwenye timu wakati Taifa Stars ilipoilaza Kenya kwa bao 1-0 kaztika mechi ya kirafiki iliyofanyika mapema mwezi huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Hata hivyo kupatikana kwao kuichezea timu ya taifa kumekuwa kwa nadra sana na hivi karibuni TFF ilieleza kuwa itashughulikia suala la wachezaji hao pamoja na Adam Nditi anayechezea timu ya vijana ya Chelsea kwa njia ya mazungumzo badala ya kutumia sheria za FIFA baada ya kushauriwa na vyama vya nchi nyingine vyenye wachezaji nyota barani Ulaya.

No comments:

Post a Comment