'
Saturday, December 1, 2012
TENGA:MAZUNGUMZO YETU NA TRA YANAKWENDA VIZURI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema ana matumaini kuwa sakata la hatua ya Mamlaka ya Mapato (TRA)kuzuia akaunti za Shirikisho litaisha mapema baada ya kumalizika kwa mkutano baina ya pande husika uliofanyika juzi.
“Pande zote tatu zimeonyesha dhamira ya kumaliza tatizo hili mapema iwezekanavyo,” alisema Tenga baada ya kumalizika kwa kikao baina ya TFF, TRA na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo.
“Kikao kimekubaliana hatua muafaka za kuchukua ili kumaliza tatizo hilo mapema kwa mujibu wa taratibu za TRA. Tutaendelea ”
TRA imeshikilia akaunti za TFF ikidai kuwa Shirikisho hilo linatakiwa kulipa kodi inayofikia jumla ya Sh 157,407,968/- ikiwa ni makato ya Kodi ya Kadri ya Mapato ya Mfanyakazi (P.A.Y.E) kwa makocha Marcio Maximo, Rodrigo Stockler de Feitas na Jan Poulsen.
Makocha hao waliletwa nchini kwa ajili ya kuzifundisha timu za taifa kutokana na ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete ya mwaka 2005 ya kuwalipa mishahara makocha wa timu za taifa ikiwa ni mchango wake katika kuendeleza michezo. Makocha hao wanalipwa na Wizara ya Michezo.
Katika sakata hilo la muda mrefu, TFF imekuwa ikijitetea kuwa mikataba ya makocha hao inaonyesha dhahiri kuwa mlipaji wa mishahara yao ni serikali na kwamba Shirikisho ni msimamizi tu wa ajira yao licha ya kwamba Shirikisho linaonekana kuwa ni muajiri wa wataalamu hao kwa mujibu wa mikataba hiyo.
Katika kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo iliyo jengo la Jubilee Tower, TFF iliongozwa na Rais Tenga wakati TRA iliongozwa na Catherine X. Nkelebe ambaye ni meneja wa mkoa wa Ilala wa mamlaka hiyo.
Pamoja na kujitetea kuwa mlipaji mshahara ndiye anayetakiwa kulipa kodi ya P.A.Y.E, TFF pia imeeleza bayana kuwa haina uwezo wa kulipa fedha hizo na kwamba fedha zilizochukuliwa ni za udhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom ambazo hutolewa kwa shughuli maalum.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment