KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, December 5, 2012

DIAMOND AMFAGILIA DULLY SYKES



MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amemfagilia mkongwe wa fani hiyo, Dully Sykes kwa kumwelezea kuwa, kwake ndiye kila kitu.
Diamond ameandika kwenye tovuti yake wiki hii kuwa, Dully ana mchango mkubwa katika safari yake ya kimuziki hadi alipofikia sasa.
"Kiukweli Dully Sykes ni mtu, ambaye ana mchango mkubwa sana katika safari yangu ya kimuziki mpaka kufikia hapa. Pengine pasingekuwa na uwepo wake, huenda nisingefika hapa nilipo,"alisema Diamond kupitia tovuti yake.
"Ni mtu anaye niunga mkono na kuwa nami bega kwa bega kwa kila hatua zangu za kimuziki, kunishauri na kuniongoza katika njia sahihi katika tasnia hii ya muziki wetu na maisha kwa ujumla," ameongeza Diamond.
Desemba Mosi mwaka huu, Dully alipata mtoto mwingine wa kiume, aliyezaliwa katika hospitali ya Greenwich ya mjini London, Uingereza na kumwita kwa jina la Diamond Sykes.
Wakati huo huo, msanii nyota na mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Dully Sykes ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Utamu.
Dully, ambaye ni maarufu kwa jina la Mr. Misifa, amerekodi kibao hicho kwa kushirikiana na wasanii machachari, Naseeb Abdul 'Diamond' na Ommy Dimpoz.
Tayari video ya wimbo huo imeshakamilika kuanza kuonyeshwa kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.
Wimbo huo umekuwa gumzo kubwa kwa mashabiki wa muziki nchini kutokana na kupigwa katika miondoko ya aina yake, lakini yenye mvuto na ladha murua masikioni.
Video ya wimbo huo pia imetayarishwa kwa ufundi wa hali ya juu na kuifanya ivutie kuitazama mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment