KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 10, 2014

TWANGA PEPETA YAINGIA MKATABA NA PRAIN PROMOTIONS


BENDI ya muziki wa dansi nchini ya African Stars 'Twanga Pepeta',
wameingia mkataba maalumu na kampuni ya Prain Promotions
Limited kwa ajili ya utengenezaji wa kazi zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, alisema mkataba
huo una manufaa kwa bendi hiyo kutokana na kutaka
kuwanufaisha wanamuziki na wasanii wa nchini kwa ujumla.

Baraka alisema kampuni hiyo ambayo awali ilikuwa
ikijishughulisha na usambazaji wa kazi za filamu, imeamua kuingia
mkataba na bendi yake kutokana na ubora wao.

Alisema wasanii nchini wanatakiwa kunufaika na kazi
wanayoifanya, na Prain wameihakikishia Twanga kuwa kazi zao
sasa zimetengenezwa kwa ubora wa hali ya juu kiasi cha
kumshinda mtu yeyote kuirudufu.

"Tunataka maendeleo ya wasanii, tumekuwa tukiwakumbatia
zaidi wasanii wa nje, lakini muunganiko wetu sasa utasaidia kuinua
hali ya kipato sahihi kwa wanamuziki tulionao," alisema Baraka.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Prain Promotions, Evance
Steven, alisema kampuni yao imeamua kuingia kwenye muziki na
kuichagua Twanga Pepeta kuwa bendi ya kwanza kutokana na
kazi yao wanayofanya katika burudani.

Steven alisema kazi kubwa waliyoanza nayo katika albamu ya
Twanga Pepeta ya Dunia Daraja ni kuhakikisha kuwa haiwezi
kunakiliwa (kurudufiwa) upya na maharamia wa kazi za kisanii
nchini kama ilivyozoeleka.

"Tumewahakikishia wenzetu wa Twanga Pepeta kuwa kazi zao
sasa ziko salama kuuzwa kihalali kutokana na kuziwekea programu
maalumu ya kushindwa kunakilika, hivyo kila mtu atanunua
kihalali kazi za bendi hii za Dunia Daraja," alisema ofisa huyo.

Twanga itaanza kuuza kazi hizo katika kila maonesho yao huku
zikionekana kufungwa katika ubora wa hali ya juu alipokuwa
akiwaonesha waandishi wa habari utofauti mkubwa uliofanywa
na Prain, ambapo pia zina stika maalumu za TRA (Mamlaka ya
Mapato Tanzania).

No comments:

Post a Comment