KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 30, 2014

KAVUMBAGU ATUA AZAM


AZAM FC, mabingwa wa Tanzania Bara wameingia Mkataba wa mwaka mmoja na Nahodha wa Burundi, Didier Kavumbangu wenye kipengele cha kuongezewa mwaka mwingine, iwapo atafanya vizuri katika mwaka wake wa kwanza.

Mshambuliaji huyo aliyemaliza Mkataba wake wa miaka miwili na waliokuwa wapinzani wakuu wa Azam FC katika mbio za ubingwa msimu huu, Yanga SC, amesaini mchana wa leo mbele ya Katibu Mkuu wa klabu, Nassor Idrisa makao makuu ya klabu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Katibu Nassor alisema; “Tumepata mshambuliaji mzuri, ambaye tayari ana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya Tanzania kwa misimu miwili, mchezaji huyu ni chaguo la kocha wetu Joseph Omog, ambaye alivutiwa naye baada ya kumuona akichezea klabu yake zamani, Yanga SC.”

Kwa upande wake, Kavumbangu alisema; “Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira. Nimemaliza mkataba Yanga, lakini viongozi hawaniambii kitu, nimepata ofa nzuri Azam nikaamua kusaini,”.

Mshambuliaji huyo mrefu mwenye nguvu amesema sasa akili yake anaipeleka kwa mwajiri wake mpya, Azam FC ambako pia amepania kwenda kushinda mataji na kuiwezesha timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika.

“Mimi sasa ni mchezaji wa Azam, nafurahi kujiunga na klabu hii kubwa. Kawaida yangu huwa nashabikia klabu nayochezea, sasa mimi ni mshabiki namba moja wa Azam,”amesema.

Kavumbangu alitua Yanga mwaka 2013 akitokea Atletico ya Burundi na katika mechi misimu miwili ya kuichezea klabu hiyo, amefunga mabao 31 katika mechi 63 za mashindano yote, moja tu la penalti.

No comments:

Post a Comment