KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 14, 2014

KOCHA OMOG WA AZAM FURAHA TUPU


KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog amefurahia ushindi wa jana wa mabao 2-1

dhidi ya wenyeji Mbeya City Uwanja wa Sokoine ulioihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara timu yake, Azam FC, lakini amewaambia wachezaji wake, pati
ni baada ya mechi ya mwisho Aprili 19, mwaka huu.

“Ni furaha sana, tumepambana sana, haikuwa kazi nyepesi, tumepitia mechi ngumu
tangu naanza kazi hapa, lakini tulibaki kwenye dhamira yetu na tukaendelea kupambana
hatimaye tumetimiza malengo. Sote tuna furaha sasa, kila mtu ana sababu ya kufurahia
kazi yake kati yetu,”alisema Omog.

Omog amewataka wachezaji wake kutobweteka na matokeo ya jana, na badala yake
waelekeze nguvu zao katika mchezo wa Aprili 19, ili washinde na kukabidhiwa Kombe
kwa furaha. “Nasikia Yanga walikata rufaa, hata kama haina maana, lakini lazima
tushinde mechi ya mwisho, wachezaji wangu wanajua hilo, nimewaambia,”alisema.

Mabao ya Gaudence Mwaikimba na John Bocco ‘Adebayor’ kila kipindi jana yalitosha
kuihakikishia Azam FC ubingwa wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya dhidi ya
bao la Mwagane Yeya.

Ushindi huo, umeifanya Azam ifikishe pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi
ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka
huu.

Nafasi ya pili tayari ni Yanga SC yenye pointi 55 sasa baada ya jana kuifunga JKT
Oljoro 2-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ambayo kama itawafunga pia na
Simba SC wiki ijayo itafikisha pointi 58, ambazo haziwezi pia kufikiwa na timu za chini
yake.

Azam FC itacheza mechi ya mwisho nyumbani, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Jumamosi wiki hii, dhidi ya JKT Ruvu ikiwa na
dhamira ya kushinda ili kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza
mechi.

Kikosi cha Azam kinaondoka leo Saa 10:00 mjini Mbeya kwa ndege kurejea Dar es
Salaam na wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja kabla ya kukutana kwa
maandalizi ya mchezo wa kufungia pazia la msimu.

No comments:

Post a Comment