KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 14, 2014

JK ATUMA RAMBIRAMBI KIFO CHA GURUMO

RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutokana na kifo cha mwanamuziki maarufu na wa siku nyingi, Muhidini Gurumo kilichotokea juzi mjini Dar es Salaam.

Gurumo alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete alisema mchango wa marehemu Gurumo kwa Taifa ni mkubwa na wa kupigiwa mfano kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia Taifa hili kwa bidii tangu miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki,

Katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013,”alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Gurumo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa familia yao.

Alisema anaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huo mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote, na anamuomba Mwenyezi Mungu.

Aliwaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi ya mola.

0000
National Arts Council BASATA

Yah: Salaam za Rambirambi

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii nguli wa tasnia ya muziki wa Dansi nchini Muhidini Maalimu Ngurumo

“ Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Muhidini Maalimu Ngurumo ambaye mchango wake katika muziki wa dansi ni mkubwa mno na unahitajika sana, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii.” Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha tunawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.

Mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Imetolewa na
Godfrey Mngereza
Kaimu Katibu Mtendaji
Baraza la Sanaa la taifa.

No comments:

Post a Comment