'
Friday, July 16, 2010
Igangula atangaza vita dhidi ya makomandoo
MGOMBEA uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga, Mbaraka Igangula amesema, iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo, hatatoa nafasi kwa wanachama maarufu kwa jina la ‘makomandoo’ kukaa milangoni wakati wa mechi za ligi.
Akizungumza na wanachama wa Yanga wa matawi ya Magomeni, Manzese na Tandale mjini Dar es Salaam juzi, Igangula alisema kazi ya kusimamia mapato ya mechi za ligi itafanywa na wanachama wa matawi. “Napenda kuliweka wazi hili kwamba, iwapo nitachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Yanga, ‘makomandoo’ hawatakuwa na nafasi katika kudhibiti mapato. Kazi hii itafanywa kwa zamu na wanachama wa matawi yote ya Yanga ya Dar es Salaam na watalipwa siku hiyo hiyo,”alisema.
Igangula alisema pia kuwa, asingependa kuiona Yanga ikiwa na viongozi wasiokuwa na kazi na ambao wamekuwa wakiitegemea klabu hiyo kuendesha maisha yao.
Alisema viongozi wa aina hiyo hawapaswi kupewa nafasi kwa sababu badala ya kuiendeleza klabu, watafanya kila njia ili kuitumia kupata fedha za kujikimu.
Mgombea huyo amewaonya pia wanachama wa Yanga wasichague viongozi, ambao wamekuwa wakiwanyonya wachezaji wa timu hiyo kwa kuwaomba pesa ama kuwakata sehemu fulani ya pesa katika malipo yao.
“Wapo baadhi ya viongozi, ambao wamekuwa wakiwaomba wachezaji ‘teni pasenti’ katika malipo yao ya usajili, mishahara na posho mbalimbali. Hawa nao hawatakuwa na nafasi Yanga,”alisema.
Igangula alisema, klabu hiyo inapaswa kuwa na uongozi imara utakaozingatia katiba, kanuni, sera na misingi ya demokrasia katika kuendesha shughuli zake.
Alisema iwapo hayo yatafanyika, itakuwa rahisi kwa wanachama wa Yanga kuwa na umoja, uwazi, usawa, uhuru na kuwepo kwa uwajibikaji katika kuendeleza michezo.
Aliitaja mikakati yake mingine kuwa ni kuhakikisha Yanga inakuwa imara kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ili kuendesha shughuli zake kiufanisi na kutoa huduma kwa wanachama na wachezaji wake.
Alisema Yanga ni klabu kubwa na yenye mahitaji mengi makubwa, hivyo inapaswa kuongozwa na viongozi bora wenye sifa katika kuleta maendeleo ya soka na utawala.
“Kiongozi wa Yanga anapaswa kuwa na kazi ya kuaminika, inayompa kipato cha maisha yake, ili asiitegemee Yanga kumuendeshea maisha yake.
“Pia anapaswa kuwa mwaminifu na mwenye rekodi safi ya kuaminiwa, hasa katika masuala ya fedha, awe na uwezo wa kuongoza, aliyeiva kiungozi na mwenye uwezo wa kubuni miradi yenye kuipa fedha Yanga,”alisema Igangula na kusisitiza kuwa anazo sifa hizo na nyinginezo hivyo anastahili kuiongoza Yanga.
Igangula aliwaahidi wanachama wa matawi hayo kuwa, iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo, atarejesha michezo ya wanawake, darts, snuka, ngumi na pia kuimarisha timu za vijana wa umri mbalimbali.
Mgombea huyo alijigamba pia kuwa, chini ya uongozi wake, atahakikisha Yanga inarejesha ubabe wake kwa Simba kwa vile hafurahishwi kuona timu hiyo ikifungwa mara kwa mara na wapinzani wao hao wa jadi.
“Nilipokuwa Kaimu Rais wa Yanga mwaka 2003, tuliweza kuifunga Simba, hivyo uwezo wa kuwafunga tena watani wetu hao ninao, nichagueni ili turejeshe ubabe wetu kwa Simba,”alisema.
Igangula aliahidi kuendeleza ujenzi wa uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani, Dar es Salaam, ambao alisema alishaandaa ramani na kuikabidhi kwa uongozi unaomaliza muda wake, lakini ameshangaa kuona hakuna kilichofanyika.
Alisema aliandaa ramani hiyo baada ya kuombwa kufanya hivyo na Mweka Hazina wa zamani wa Yanga, Abeid Abeid kwa ahadi kwamba angesimamia ujenzi wa uwanja huo. Abeid ni mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo.
Aliitaja mikakati yake mingine ndani ya Yanga kuwa ni kuondoa makundi miongoni mwa wanachama na kuimarisha nidhamu kwa wachezaji.
Alisema chini ya uongozi wake, atahakikisha wachezaji wanalipwa kutokana na kujituma kwao na kusisitiza kuwa, hakutakuwa na tofauti kubwa ya mishahara kati ya wachezaji wazalendo na wa kigeni.
“Ninachowaomba wanachama wenzangu ni kunipa ushirikiano na kuepuka kuchagua viongozi waliowahi kuvurunda miaka ya nyuma kwa sababu hawatakuwa na kipya,”alisema.
Igangula pia aliahidi kuwa karibu zaidi na wazee wa klabu hiyo kwa vile ndio wanaoifahamu vyema Yanga na busara zao zinapaswa kutumika katika kuiendeleza.
Mgombea huyo aliahidi kuitisha mara kwa mara mikutano ya wanachama na kuwapa nafasi ya kutoa mchango wa mawazo yao kwa lengo la kuifikisha mbali zaidi klabu hiyo.
Alisema kamwe hatokuwa mwoga wa kuitisha mikutano ya wanachama kama ilivyokuwa kwa viongozi wengi waliopita kwa vile kufanya hivyo ni kuwanyima nafasi wanachama ya kuitumikia klabu yao.
Igangula ni mmoja wa wagombea watano waliopitishwa kuwania wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa Yanga, unaotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye ukumbi wa PTA uliopo kwenye viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Wagombea wengine wa nafasi hiyo ni rais wa zamani wa klabu hiyo, Francis Kifukwe, Abeid Abeid, Llyord Nchunga na Edgar Chibula
Igangula, aliwahi kuwa makamu wa rais wa Yanga mwaka 2001 hadi 2003. Pia alikuwa kaimu rais wa Yanga mwaka 2003 na mwenyekiti wa kamati ya muafaka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment