KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, July 16, 2010

Naomi Campbell kutoa ushahidi kesi ya Taylor



LONDON, Uingereza
MWANAMITINDO nyota duniani, Naomi Campbell anatarajiwa kutoa ushahidi mbele ya mahakama ya kimataifa katika kesi ya uhalifu wa kivita, inayomkabili Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor.
Msemaji wa mwanamitindo huyo, alisema juzi kuwa, Naomi anatarajiwa kutoa ushahidi huo Julai 29 mwaka huu katika mahakama ya The Hague.
Taylor anatuhumiwa kutumia almasi kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea nchini Sierra Leone na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.
Waendesha mashtaka katika kesi hiyo wamemtaka Naomi kutoa ushahidi kuhusu tuhuma kwamba, alipokea madini ya almasi kutoka kwa Taylor mwaka 1997.
“Yeye ni shahidi, ambaye ametakiwa kusaidia kuthibitisha matukio yaliyotokea mwaka 1997. Naomi ameeleza wazi kuwa, yupo tayari kusaidia sheria ichukue mkondo wake,”alisema msemaji wa mwanamitindo huyo.
“Kwa kuondoa wasiwasi wowote, (Naomi) hatuhumiwi kufanya lolote baya na hahusiki na kesi hiyo,”aliongeza.
Waendesha mashtaka katika kesi hiyo wanataka kufahamu iwapo Naomi alipokea madini ya almasi kutoka kwa Taylor katika hafla iliyoandaliwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela nchini humo mwaka 1997.
Awali, msemaji wa mahakama hiyo alisema Naomi alikanusha kupokea madini kutoka kwa Taylor na alikataa kuzungumza na waendesha mashtaka.
Akihojiwa katika kipindi cha Oprah Winfrey Show, Naomi hakuwa tayari kuthibitisha ama kukanusha kwamba alipokea madini hayo, badala yake alisema: “Sitaki kuhusishwa katika kesi ya mtu huyu. Amefanya baadhi ya mambo ya kutisha na sitaki kuiingiza familia yangu kwenye hatari.”
Mbali na Naomi, mwigizaji nyota wa filamu wa Marekani, Mia Farrow naye huenda akatoa ushahidi katika kesi hiyo. Mia ndiye anayedaiwa kumweleza Naomi kuhusu zawadi hiyo ya madini.
Taylor ameshakanusha tuhuma za mashtaka 11 aliyoshtakiwa katika kesi hiyo. Kesi hiyo imeshachukua zaidi ya miaka miwili tangu ilipoanza kusikilizwa.
Kiongozi huyo wa zamani wa Liberia, anatuhumiwa kuuza madini ya almasi na kununua silaha kwa ajili ya magaidi wa RUF wa Sierra Leone, ambao waliendesha vita vilivyosababisha kukatwa mikono na miguu kwa raia kadhaa wan chi hiyo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea kati ya mwaka 1991 hadi 2001.

No comments:

Post a Comment