TAKUKURU yawawekea mitego wagombea
WAKATI wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu ya Yanga wameanza kampeni, umezuka mchuano mkali kati ya wagombea wawili wa nafasi ya mwenyekiti, Mbaraka Igangula na Francis Kifukwe.
Kuzuka kwa mchuano huo kumekuja baada ya Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumrejesha Kifukwe kwenye uchaguzi huo baada ya awali kutemwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga.
Kifukwe na mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Abeid Abeid waliondolewa kwenye uchaguzi huo baada ya kuwekewa pingamizi na baadhi ya wanachama wa Yanga.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, Igangula na Kifukwe ndio pekee wanaoungwa mkono na wanachama wa Yanga kutokana na kuiongoza klabu hiyo kwa nyakati tofauti miaka ya nyuma.
Kutokana na wagombea hao kuwa na wafuasi wengi, wanachama wa Yanga kwa sasa wamewanyika makundi mawili, kila moja likiwafanyia kampeni wagombea hao wawili kwa ajili ya kushika nafasi hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa, Igangula ndiye mwenye wafuasi wengi, ambao wamekuwa wakitembelea matawi mbalimbali ya klabu hiyo kwa ajili ya kumfanyia kampeni.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Igangula anakubalika katika matawi mengi ya pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam wakati Kifukwe anakubalika na wanachama wa makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani.
Igangula aliwahi kuwa makamu wa rais wa Yanga chini ya uongozi wa Tarimba Abbas kabla ya kuteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo na baadaye kupinduliwa na wanachama.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kigoma jana, Igangula alisema amejipanga vyema kuhakikisha anaitwaa nafasi hiyo kwa vile ana uzoefu wa muda mrefu wa uongozi ndani ya Yanga.
“Mimi nipo Kigoma kikazi, lakini ninayo timu yangu inayoondesha kampeni kwa ajili yangu na mambo hadi sasa yanakwenda vizuri,”alisema mgombea huyo.
Wagombea wengine wanaowania nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi huo ni Lloyd Nchunga, Abeid Abeid na Edgar Chibura.
Mchuano mwingine mkali upo kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti, inayowaniwa na Ayoub Nyenzi, Constantine Maligo na Davis Mosha. Katika nafasi hiyo, wagombea wanaoonekana kuungwa mkono na wanachama wengi ni Nyenzi na Mosha.
Waliopitishwa kuwania nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji katika uchaguzi huo ni Yusuf Yasin, Robert Kasela, Shaaban Mohamed, Omary Ndula, Atufwigwegwe Mwakatumbula, Evance Matee, David Peter, Majid Simba, Mzee Yusuf, Ramadhan Kampira, Edgar Fongo, Jackson Maagi, Mwinyi Mangara, Hamis Ambari na Mohamed Bhinda.
Wengine ni Isaac Mazwile, Paul Malume, Sarah Ramadhan, Salim Rupia, Dk. David Ruhago, Titto Ossoro, Charles Mugondo, Ally Mayay, Pascal Kihanga, Ismail Idrissa, Lameck Nyambaya, John Mayala, Theonest Rutashoborwa na George Manyama.
Uchaguzi mkuu wa Yanga umepangwa kufanyika Julai 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa PTA uliopo kwenye viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, John Mkwawa alitangaza juzi kuwa, kampeni kwa wagombea zilipaswa kuanza rasmi jana hadi Julai 17 mwaka huu.
Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imesema, imeanza kuwafuatilia kwa karibu wagombea wa uongozi katika klabu ya Yanga kwa lengo la kuwashughulikia watoa rushwa.
Mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo alisema jana kwa njia ya simu kuwa, mgombea yeyote atakayekamatwa akitoa rushwa kwa wanachama, atachukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment