MWIMBAJI machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Khadija Shaaban ‘K-Sher’ amesema anapenda sana kuimba nyimbo zinazohusu mapenzi kwa lengo la kuisaidia jamii.
Akizungumza katika kipindi cha Friday Nite Live kilichorushwa hewani na luninga ya East Africa mwishoni mwa wiki iliyopita, K-Sher alisema nyimbo za aina hiyo zinagusa maeneo mbalimbali ya maisha ya jamii.
K-Sher alisema kamwe hapendi kuimba nyimbo zinazozungumzia matukio yaliyowahi kumkuta katika maisha yake kama wanavyofanya wasanii wengine wa muziki huo.
Mbali na kupendelea zaidi kuimba nyimbo za mapenzi, msanii huyo alisema baadhi ya nyimbo zake hutungiwa na wasanii wengine. Alitoa mfano wa nyimbo hizo kuwa ni ‘Usinicheke’, uliotungwa na msanii Spider.
Msanii huyo aliyemaliza elimu ya kidato cha sita hivi karibuni alikiri kuwa, fani ya muziki imemuwezesha kupata manufaa mengi kimaisha ikiwa ni pamoja na uwezo kimapato.
“Namshukuru Mungu kuwa kwa sasa nina uwezo wa kununua nguo ya thamani yoyote, lakini kuna vitu ambavyo nimekuwa nikivipa kipaumbele,”alisema.
K-Sher alielezea masikitiko yake kuona kuwa, wapo baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ambao wamekuwa wakitunga na kuimba nyimbo za kuvutia, lakini hawapati mafanikio.
Alisema cha ajabu ni kuona kwamba, wale wasanii wanaotunga na kuimba nyimbo kwa mipigo ile ile ndio wanaopata mafanikio na kuvuma pembe zote za nchi.
“Sijui tuseme watanzania hawaujui muziki! Inashangaza kuona msanii anaimba nyimbo kwa melody ileile, lakini nyimbo zake zinavuma sana.
“Lakini wapo wanaoimba nyimbo zao kwa melody tofauti na kutoa ujumbe mzito kwa jamii, lakini nyimbo zao hazikubaliki,”alisema msanii huyo.
Alimmwagia sifa kemkem msanii mwenzake wa kike, Vumilia kwa kuimba nyimbo zenye mvuto na ambazo alisema si rahisi kuchujuka baada ya muda mfupi.
“Kwa kweli namzimia sana Vumilia. Tazama nyimbo zake za ‘Utanikumbuka’ na ‘Kama ni umaskini’. Ni nyimbo zenye mvuto, mashairi yake yanavutia na sauti yake ni tamu kuisikiliza,”alisema.
Alisema binafsi kila anapoamka asubuhi na kukerwa na jambo fulani, huwa anapenda kusikiliza nyimbo hizo kwa vile zinamfariji na kumpa liwazo murua.
Pamoja na mafanikio kadhaa yaliyopatikana kwa wasanii nchini kutokana na muziki huo, K-Sher alisema si rahisi kwa muziki wao kudumu kwa muda mrefu.
Aliufananisha muziki wa kizazi kipya kuwa ni sawa na utamu wa Big G, ambayo baada ya kutafunwa kwa muda mfupi, humalizika na kuwa haina ladha tena.
“Hivi ndivyo muziki wetu ulivyo. Ni sawa na Big G. Ukishaitafuna na utamu kumalizika, haina ladha tena mdomoni,”alisema.
Kwa sasa, msanii huyu anatamba kwa kibao chake kipya kinachojulikana kwa jina la ‘Nastahili kupendwa’, ambacho ni miongoni mwa vibao vipya vitakavyokuwemo kwenye albamu ya kundi la Tip Top Connection.
Kundi hilo linajiandaa kufanya ziara katika mikoa kadhaa nchini kwa ajili ya kuitangaza albamu hiyo, itakayowajumuisha wasanii wengine kama vile Madee, Tundaman, Cassim Mganga na Dezo.
Mbali na kuitangaza albamu hiyo mikoani, K-Sher alisema kundi hilo pia linatarajia kufanya ziara katika nchi jirani za Kenya na Uganda.
K-Sher alisema japokuwa kundi lao lipo chini ya Meneja Babu Tale, wao ndio kama waajiri wake kwa sababu ndio wanaofanyakazi zinazomwezesha kupata kipato.
“Sisi ndio mameneja wa Babu Tale kwa sababu ndio tunaotoa kazi na kumlipa,”alisema.
No comments:
Post a Comment