KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 1, 2010

Ni Brazil vs Uholanzi, Ghana vs Uruguay



Mensah, Sarpei, Boateng hatarini kucheza
Dunga akiri pambano litakuwa gumu kwao
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MICHUANO ya soka ya fainali za Kombe la Dunia, inaingia katika hatua ya robo fainali leo wakati timu nne zitakapoteremka dimbani katika viwanja viwili tofauti.
Katika mechi hizo, Brazil itamenyana na Uholanzi kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Port Elizabeth wakati Ghana itavaana na Uruguay kwenye uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.
Brazil ilifuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuichapa Chile mabao 3-0 katika raundi ya pili wakati Uholanzi ilitinga robo fainali baada ya kuishinda Slovakia mabao 2-1.
Nao wawakilishi pekee wa Afrika waliosalia katika fainali hizo, Ghana walifuzu kucheza robo fainali baada ya kuichapa Marekani mabao 2-1 wakati Uruguay iliitoa Korea Kusini kwa idadi hiyo ya mabao.
Pambano kati ya Brazil na Uholanzi ndilo linalovuta hisia za mashabiki wengi wa soka duniani, kufuatia timu hizo kuonyesha kandanda ya kuvutia tangu michuano hiyo ilipoanza Juni 11 mwaka huu.
Kocha Mkuu wa Brazil, Carlos Dunga alikiri juzi kuwa, pambano hilo litakuwa gumu kwao kutokana na kiwango cha juu kilichoonyeshwa na Uholanzi katika hatua za awali.
“Tunaelewa Uholanzi ni timu ngumu kuifunga na kucheza nayo,”alisema Dunga. “ Mchezo wao hauna tofauti na soka ya Amerika ya Kusini. Hawachezi soka ya kujihami na hutumia pasi ndefu. Wanacheza soka ya ufundi na tutalazimika kuwa tayari kukabiliana nao.”
Brazil haijakumbana na timu ngumu hadi sasa. Ilitwaa uongozi wa kundi G baada ya kuzifunga Korea Kaskazini mabao 2-1, ikaichapa Ivory Coast mabao 3-1 kabla ya kutoka suluhu na Ureno.
“Sasa ni mechi kati ya timu mbili zenye utamaduni tofauti wa kucheza soka na zenye wachezaji wa kiwango cha juu,” alisema nahodha wa Brazil, Lucio.
Beki huyo mkongwe kwenye kikosi cha Brazil alikiri kuwa, kadri michuano hiyo inavyosonga mbele, mechi zinakuwa ngumu zaidi.
Uholanzi haijawahi kutwaa Kombe la Dunia, lakini imefanya vizuri katika mechi za mzunguko wa kwanza kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Denmark, Japan, Cameroon na Slovakia.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Brazil kukutana na Uholanzi katika michuano ya Kombe la Dunia, ambapo Brazil ilishinda mechi mbili na kufungwa moja.
Uholanzi iliishinda Brazil katika raundi ya pili ya michuano ya mwaka 1974 nchini Ujerumani kabla ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 katika robo fainali mwaka 1994. Brazil pia iliishinda Uholanzi hatua ya nusu fainali katika michuano ya mwaka 1889 iliyofanyika Ufaransa.
Katika mechi hiyo, Brazil huenda ikawakosa viungo wake, Elano na Felipe Melo, ambao ni majeruhi. Elano alishindwa kufanya mazoezi Jumanne iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.
Brazil pia itamkosa Ramires, aliyechukua nafasi ya Melo, kufuatia kuwa na kadi mbili za njano.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Uholanzi, Bert van Marwijk alisema ni vigumu kutabiri pambano hilo kwa vile timu hizo mbili zina historia ya kufungana kwa zamu.
Tegemeo kubwa la Uholanzi litakuwa kwa washambuliaji wake, Robin van Persie, Ryan Babel, Dirk Kuyt na Arjen Robben.
Wasiwasi wa Ghana kumkosa mshambuliaji wake nyota, Asamoah Gyan umepungua baada ya mchezaji huyo juzi kufanya mazoezi na wenzake.
Asamoah, nahodha John Mensah, kiungo Kevin Prince Boateng na beki Hans Sarpei walishindwa kufanya mazoezi mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu.
Kocha Milovan Rajevac wa Ghana alisema juzi kuwa, Mensah anasumbuliwa na maumivu ya mgongo na hawezi kufanya mazoezi na amekuwa akisaidiwa na daktari maalumu kutoka Ufaransa.
Boateng aliumia mkono katika mechi dhidi ya Marekani na amekuwa akipatiwa tiba maalumu ili awemo kwenye kikosi kitakachocheza na Uruguay.
Uwezekano wa Sarpei kucheza mechi ya kesho ni mdogo kutokana na kuumia mguu na Rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyanyakyi alithibitisha kuwa beki huyo hatacheza.
Milovan alisema pengo la Mensah litazibwa na beki Isaac Vorsah, lakini hana hakika kama Sulley Muntari anaweza kucheza nafasi ya Dede Ayew mwenye kadi mbili za njano.
Kocha Mkuu wa Uruguay, Oscar Tabarez alisema hawawezi kuidharau Ghana kwa vile imeonyesha soka ya kiwango cha juu katika mechi zake zilizopita na imepania kuweka historia mpya kwa bara la Afrika.
Tegemeo kubwa la Oscar katika mechi hiyo litakuwa kwa washambuliaji wake nyota, Diego Forlan, Luis Suarez na Jorge Martinez.

No comments:

Post a Comment