KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, July 16, 2010

K-SHYINA: Acheni kutukatisha tamaa wasanii chipukizi



KWA kawaida, safari ya wasanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini hutawaliwa na vikwazo vingi, vikiwemo kukatishwa tamaa na nyimbo zao kuibwa na wasanii wakongwe.
Lakini vikwazo vikubwa zaidi ni kukosa uwezo wa kurekodi nyimbo zao studio kutokana na kutokuwa na pesa ama watangazaji wa vipindi vya muziki kutopiga nyimbo zao hadi wapewe ‘kitu kidogo’.
Hayo ndiyo matatizo yanayomkuta msanii chipukizi wa muziki huo, Kelvin Stephano, ambaye ni maarufu kwa jina la K-Shyina, mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam.
Licha ya kutunga na kurekodi kibao kitamu na chenye mashairi yenye mvuto, kinachokwenda kwa jina la ‘Uzuri wa sura’, K-Shyina hajawahi kusikika hata siku moja kwenye vituo vya radio.
Kila anapopeleka CD za wimbo huo kwenye vituo mbalimbali vya radio, hupewa ahadi za ‘kitapigwa kesho’, lakini siku zinakwenda bila kibao hicho kusikika.
Adha hiyo ni ya pili kumkumba msanii huyo mwenye umri wa miaka 20. Adha ya kwanza ilikuwa ‘kuliwa’ pesa zake kila alipokwenda studio kulipia gharama za kurekodi wimbo huo.
“Nimeshawahi kuliwa pesa zangu mara nne katika studio tofauti, kubwa na ndogo. Nilikuwa napewa ahadi ya ‘njoo kurekodi kesho’ hadi nikakata tamaa na kuzisamehe pesa zangu,”alisema msanii hiyo alipozungumza na Burudani wiki hii mjini Dar es Salaam.
Mbali na kuliwa pesa zake, K-Shyina alisema amekuwa akikutana na kauli mbalimbali zenye lengo la kumkatisha tamaa katika safari yake hiyo ya kimuziki.
“Wasanii tunaochipukia tumekuwa tukikumbana na kauli nyingi za kutukatisha tamaa, hasa katika maeneo tunayoishi. Utakuta wengine wanakwambia, ‘kuimba anaimba, lakini kutoka hatoki’. Kauli hizi zinakatisha tamaa, lakini sikubali kushindwa,”alisema.
Msanii huyo aliitaja adha nyingine inayowakumba wasanii chipukizi kuwa ni pamoja na kuibwa kwa nyimbo zao, pale wanapowafuata wasanii wakongwe ili wawape msaada wa kiusanii.
“Ukimfuata msanii mkongwe kumuomba msaada, anaweza kukwambia ‘hebu niimbie wimbo wako’. Baada ya siku mbili tatu, utausikia wimbo huo redioni ukiwa umebadilishwa mashairi, lakini sauti ni ileile,”alisema. K-Shyina (18) alikiri kuwa, bila ya kuwa na mdhamini, ni vigumu kwa msanii chipukizi kuweza kupata mafanikio katika muziki huo kwa sababu gharama za kurekodi wimbo mmoja ni kubwa.
Amewataka wasanii nchini kupendana na kujenga tabia ya kusaidiana, badala ya kukatishana tamaa ama kujenga chuki baina yao.
“Nawaomba wasanii, ambao kwa sasa wapo juu, watusaidie sisi tuliopo chini badala ya kutuvunja nguvu ama kutuibia nyimbo zetu,” alisema msanii huyo mwenye elimu ya sanaa aliyoipata katika kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
“Nawaomba pia wasanii wenzangu, tuwe mfano wa kuigwa na jamii kwa kuielimisha juu ya mambo mbalimbali muhimu, lakini tunapofanya hivyo, isiwe tena sisi ndio watendaji wa hayo mambo,”aliongeza. Pia amewataka wasanii chipukizi wasikatishwe tamaa na vikwazo mbalimbali, ambavyo wamekuwa wakikutana navyo, badala yake waongeze bidii ya kuwasaka wadhamini ili waweze kutekeleza malengo yao.
Msanii huyo, anayevutiwa na wasanii Diamond, AY, Matonya na K-Sher alisema ameamua kujitosa kwenye fani hiyo baada ya kubaini kuwa, ana kipaji cha kutunga na kuimba nyimbo.
Akizungumzia kibao chake cha ‘Uzuri wa sura’, alichokirekodi kwa gharama zake katika studio za Waso Records, msanii huyo alisema ni kisa cha kweli alichosimuliwa na rafiki na kilimtokea mtu anayemfahamu.
Katika kibao hicho, K-Shyina anamlalamikia mwanadada mrembo kwa sura na anayependeza kwa mavazi, lakini tabia yake mbaya ilimsababishia kuambukizwa ugonjwa hatari wa ukimwi.
“Kwa kweli hiki ndicho kibao changu cha kwanza. Ndio kwanza naanza. Bado sijajulikana na wala kupata mafanikio. Nataka niwe mwanamuziki maarufu kama walivyo wasanii wengine,”alisema.

No comments:

Post a Comment