NA AMINA ATHUMAN
MABAO mawili yaliyofungwa na Simon Msuva na Donald Ngoma
yameiwezesha Yanga kuibuka na ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara
dhidi ya Coastal Union.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
Yanga iliandika bao lake la kwanza dakika ya saba kupitia kwa Msuva aliyeachia shuti
kali akiunganisha pasi ya Kelvin Yondan.
Bao la pili lilipatikana dakika ya 42 baada ya Ngoma
kuunganisha mpira uliorudi uwanjani baada ya kipa wa Coastal Union kupangua
mpira wa krosi iliyochongwa na Msuva.
Katika mchezo huo, Yanga ilianza mchezo kwa kasi na
kushambulia lango la wapinzani wao kama nyuki ikitafuta mabao ya kufunga.
Dakika ya 12 Coastal Union ilibadilisha mfumo wa uchezaji na
wachezaji wake kurudi nyuma kwa ajili ya kuzuia mashambulizi.
Hali hiyo ilisaidia kupunguza kasi ya Yanga lakini dakika ya
18 Niyonzima alibaki na kipa Sebwato Nicholas, lakini shuti alilopiga lilitoka
pembeni kidogo ya goli.
Coastal Union ilijibu shambulizi hilo dakika ya 23 ambalo
halikuzaa matunda kabla ya kufanya mabadiliko na kumtoa Adeyum Ahmed na kuingia
Twaha Ibrahim
Mabadiliko hayo yaliamsha ari ya wachezaji wa Coastal Union
ambapo dakika ya 29 Ali Ahmed alipata nafasi ya kufunga na kuachia shuti kali
lililopaa mita chache na kutoka nje.
Coastal Union ilipata nafasi nyingine dakika ya 76 kupitia kwa
Patrick Protas baada ya kubaki na kipa lakini mpira aliopiga ulitoka pembeni
kidogo ya goli.
Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini hadi
dakika 90 zinamalizika Yanga ndiyo iliyoondoka uwanjani na kicheko baada ya
kupata pointi tatu.
Ali Mustapha, Mbuyu Twite, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin
Yondan, Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe/Malimi
Busungu, Donald Ngoma na Godfrey Mwashiuya/Deus Kaseke.
Coastal Union:Sebwato Nicholas, Hamad Juma, Yasin Mustapha,
Ernest Joseph, Tumba Sued, Said Jeilan/Patrick Protas , Ali Ahmed, Yousoufa
Sabo, Nasoro Kapama, Godfrey Wambura na Adeyum Ahmed.
No comments:
Post a Comment