KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, September 28, 2015

WASANII KIBAO KUKAMUA TAMASHA LA AMANI TAIFA

UPENDO Nkone
ROSE Muhando


NA MWANDISHI WETU

MACHO na masikio ya Watanzania yanatarajiwa kuelekezwa katika tamasha kamambe la kuombea amani ambalo limepangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Tamasha hilo ni maalumu kwa ajili ya kuwaombea amani Watanzania wanaotarajia kupiga kura za kumchagua rais wa awamu ya tano, wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia waimbaji mbalimbali maarufu kutoka Afrika watanogesha tamasha hilo kupitia vipaji vyao vya kuimba nyimbo za kumsifu Mungu.

Ingawa mfumo wa vyama vingi ulianza mwaka 1992, lakini uchaguzi wa Oktoba 25 una mvuto wa aina yake, hivyo tamasha hilo linafanyika katika muda mwafaka.

Tanzania inafanya uchaguzi wake wa tano ukitanguliwa na uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 ambao ulimuweka Rais Kikwete madarakani.

Kampuni ya Msama Promotions imeandaa tamasha hilo ili kuomba uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu ili kulinda maslahi ya Taifa na mali za Watanzania.

Tamasha hilo linatarajia kufanyika katika mikoa 10 ya Tanzania Bara ikiwemo Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga.

Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, anasema tamasha hilo lina lengo la kuwaleta pamoja Watanzania kuombea amani nchi yao katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

"Kutokana na umuhimu wa amani kampuni ya Msama Promotins inayoratibu matamasha ya muziki wa injili wakati wa Pasaka na Krismasi kila mwaka, tumeona ni vyema kuandaa tamasha hili kusisitiza amani kwa kila Mtanzania," anasema Msama.

Anasema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika na amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kumuunga mkono Rais Kikwete ambaye amekuwa mstari wa mbele kusisitiza amani.

Msama anadokeza kuwa tamasha la mwaka huu litakuwa na ujumbe “Tanzania ni ya Kwetu, Tuilinde na Kuitunza Amani Yetu.’

Anasema mustakabali wa amani ya nchi iko mikononi mwa Watanzania na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda kwa nguvu zote ili kuepuka vurugu zinazoendelea katika baadhi ya nchi duniani.

Juhudi hizi za kusisitiza amani na utulivu wa nchi hasa katika kipindi  cha uchaguzi, kinapaswa kuungwa mkono na kila mmoja kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu.

Anasema waimbaji wa nyimbo za injili wa nafasi kubwa ya kutoa mchango wao kupitia tungo za nyimbo zao zenye kujenga na kudumisha amani ya nchi.

"Waimbaji wana fursa nzuri ya kutoa mchango wao kupitia neno la Mungu, naomba Watanzania wote bila kujadili itikadi za nyama kujitokeza kwa wingi katika tamasha hili,"anasema Msama.

Mkurugenzi huyo ametoa rai kwa wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi kupiga kura kwa amani ili kulinda umoja na mshikamano wa Watanzania.

Viongozi mbalimbali wamepongeza uwepo wa tamasha hilo kwa kuwa linaitakia mema Tanzania ambapo iko katika harakati za kuchagua viongozi ambao watakaa madarakani kwa miaka mitano ijayo.

Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo kwa kuwa lina maslahi makubwa kwa Taifa.

“Viongozi wa dini ni watu muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla, wao ndio mwongozo wetu bila kuwapo wao sijui Tanzania yetu ingekuwaje”, anasema Azzan.

Waimbaji mashuhuri kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Congo na Afrika Kusini, wanatarajia 'kuchuana' vikali na wenzao wa Tanzania katika tamasha hilo.

Mwimbaji nguli wa muziki wa injili mwenye maskani yake Uingereza, Ifeanyi Kelechi, anatarajia kukonga nyoyo za Watanzania katika tamasha hilo.

Baadhi ya waimbaji watakaopanda jukwaani kutoka nje ni Anastazia Mukabwa (Kenya), Sipho Makhabane, Glorius Celebrations ‘Kwetu Pazuri’, Ephraim Sekeleti, Solomon Mukubwa na Sara K.

Kwa upande wa waimbaji wa Tanzania ni John Lissu, Boniface Mwaitege, Martha Mwaipaja, Beatrice Mwaipaja, Rose Muhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Joshua Mlelwa na Christopher Mwahangila.

No comments:

Post a Comment