'
Monday, September 21, 2015
SIMBA YAITUMIA SALAMU YANGA, YAICHAPA KAGERA SUGAR MABAO 3-1
TIMU kongwe ya soka nchini, Simba jana iliendelea kuchanua katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitandika Kagera Sugar mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji Hamisi Kiiza ndiye aliyeibeba Simba baada ya kuifungia mabao yote matatu.
Kutokana na kuzitikisa nyavu za Kagera Sugar mara tatu, Kiiza sasa ameweka rekodi ya kuifungia Simba mabao matano katika mechi tatu ilizocheza za ligi hiyo.
Simba sasa imefikisha pointi tisa sawa na Yanga na Azam, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa. Yanga inaongoza kwa mabao mengi ya kufunga.
Kiiza alifunga bao la kwanza katika kipindicha kwanza, alipounganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Awadh Juma. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipa Manyika Peter wa Simba alistahili pongezi kutokana na kuzuia mipira mingi ya hatari iliyopigwa na washambuliaji wa Kagera Sugar.
Kiiza aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 46 baada ya kumalizia krosi safi kutoka kwa beki wa kushoto, Mohamed Hussein Tshabalala.
Kagera Sugar ilipata bao la kujifariji dakika ya 50 lililofungwa na Mbaraka Yussuf baada ya mabeki wa Simba kujichanganya katika eneo lao la hatari.
Kiiza alihitimisha karamu ya magoli dakika ya 90 baada ya kuifungia Simba bao la tatu kwa shuti kali, baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto.
Simba wanatarajiwa kushuka tena dimbani Septemba 26, mwaka huu, kuvaana na mahasimu wao Yanga katika mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment