KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 31, 2017

KESI YA AVEVA, KABURU YAZIDI KUPIGWA KALENDA



UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayowakabili   Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu' umedai unaendelea na uchunguzi wa nyaraka zilizokusanywa ambazo zimepelekwa kwa mtaalamu wa maandishi.

Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson alidai hayo jama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Esterzia alidai hayo wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa ambapo aliieleza mahakama kuwa bado wanaendelea na uchunguzi wa nyaraka mbalimbali zilizokusanywa ambazo zimepelekwa kwa mtaalamu wa maandishi, hivyo wanasubiria ripoti.

Kutokana na hilo, Esterzia aliomba shauri hilo liahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu Victoria aliuhimiza upande wa jamhuri kujitahidi ili ripoti hiyo itoke mapema na kesi iweze kuendelea.

Shauri hilo liliahirishwa hadi Septemba 8, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa mahabusu kwa kuwa miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni ya kutakatisha fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, viongozi hao wa klabu ya Simba, wanakabiliwa na mashitaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha Dola za Marekani (USD) 300,000.

Washitakiwa hao   walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Aveva anadaiwa  Machi 15,2016, katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, huku akijua   alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Aveva na Nyange wanadaiwa tarehe tofauti  kati ya Machi 15 na Juni 29,2016, mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000, wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Aveva anadaiwa  Machi 15,2016, katika benki ya Baclays, Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Nyange anadaiwa Machi 15,2016, katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia USD 300,000, wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

No comments:

Post a Comment