KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 20, 2017

YAMETIMIA SIMBA


Wanachama 1,216 wa klabu ya Simba, leo wameridhia mfumo wa klabu yao kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC), Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Jinsia na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala, Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kwamba asilimia 50 ya hisa zitauzwa kwa mwekezaji yeyote au wowote watakaoungana wasiozidi watatu, kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu hiyo.

Abdallah alisema mwekezaji huyo au hao, wanatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20 ili kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu, wakati kwa kuanzia wanachama wote wa Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa.

Alisema asilimia nyingine 40 zitawekwa kama mtaji wa klabu na zitauzwa kwa wanachama baadaye, lakini wale wawekezaji walionunua asilimia 50 awali, hawataruhusiwa kununua hata hisa moja kwenye asilimia 40 za mtaji.

Na baada ya mkutano wa leo, zoezi litakalofuata ni uhakiki wa wanachama wa klabu hiyo ili kuweza kujua mgawanyo wa asilimia 10 za hisa utakavyokuwa – na itaundwa Kamati maalum ya kupitia maombi ya wawekezaji wanaotaka kununua asilimia 50 ya hisa.

Mgeni rasmi, Dk Kigwangala ameunga mkono mabadiliko hayo na kuwaambia wanachama wa Simba wamechelewa kufanya uamuzi wa mabadiliko hayo, kwani walipaswa kufanya hivyo miaka mingi iliyopita na anaamini klabu nyingine zitafuata nyayo hizo.

“Leo Agosti 20 klabu ya Simba imetengeneza rekodi nyingine baada ya ile ya mwaka 1977 ya kuwafunga Yanga 6-0, na sisi kama Serikali chini ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunaunga mkono mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu ya Simba,”amesema Dk. Kigwangala.

Kigwangala alisema serikali ya Rais Magufuli inaelewa changamoto za maendeleo ya soka na imekwishaanza kukarabati viwanja vya soka ili kukuza na kuendeleza vipaji na kuviendeleza huku ikijipanga kukusanya kodi.

Alisema rais Magufuli anapenda michezo, amefanikisha hatua za ujenzi wa uwanja wa michezo mkoani Dodoma kwa ufadhili wa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI ambao ni zaidi ya Dola za Marekani milioni 100.

Kwa upande wake Mwanasheria aliyefanikisha muundo huo mpya, Evodius Mtawala ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa klabu hiyo, alisema kwamba baada ya taratibu hizo kukamilika kinachofuata ni Kamati ya Utendaji kutengeneza kamati huru itakayosimamia tenda ambako pia baadaye itatangazwa tenda.

Naye Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura alisema mfumo uliopo katika soka la sasa ni kuendesha mchezo huo kibiashara na kuachana na mfumo wa kisiasa.

Wambura alisema wanachama wakiingia kwenye mfumo wa hisa, wataziingiza familia zao kwenye urithi endelevu hali ambayo ni tofauti na ilivyokuwa awali kwenye uanchama.

“Simba mara nyingi ndio wanakuwa wa kwanza kutekeleza maendeleo na hata ile migogoro ya mara kwa mara haitokuwepo tena na hata makomandoo hawatokuwepo, utakaposababisha Simba ipoteze mapato unajitakia njaa, mpango uliofanikishwa na Simba umeishitua TFF,” alisema Wambura.

No comments:

Post a Comment