KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 20, 2013

KAMATI YA UTENDAJI YANGA KUFUMULIWA

KAMATI ya Utendaji ya klabu ya Yanga huenda ikavunjwa na kuundwa upya baada ya wanachama wa klabu hiyo kuwapa meno mwenyekiti na makamu mwenyekiti kufanya uteuzi wa wajumbe wanaowataka.

Uamuzi huo ulifikiwa jana katika mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika kwenye bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama 1,114.

Uongozi wa Yanga uliamua kuwasilisha ombi hilo kwa wanachama ili mwenyekiti na makamu mwenyekiti wawe na uwezo wa kuteua wajumbe wa kamati hiyo na kuwatimua iwapo watashindwa kutekeleza vyema majukumu yao.

Akizungumza baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Manji alisema tayari mjumbe mmoja, ambaye hakumtaja jina ameshaenguliwa katika kamati hiyo kwa kosa la kuwatukana viongozi.

"Mwanachama yeyote atakayekwenda kinyume na muundo wa uendeshwaji wa klabu yetu tutamfukuza mara moja na lengo ni kujenga na si kubomoa," alisema Manji.

Hata hivyo, wanachama hao walikataa kupitisha ajenda ya kumpa nafasi mwenyekiti na makamu wake kupendekeza viongozi watakaochukua nafasi zao baada ya uongozi wao kumaliza muda wake.

Baada ya ajenda hiyo kukataliwa, Manji alisema utaratibu uliokuwepo awali utaendelea kutumika kama ilivyokuwa zamani na katiba haitabadilishwa.

Ajenda nyingine zote zilizosomwa katika mkutano huo zilipitishwa kwa kishindo na wanachama hao, ambao pia walipata nafasi ya kutoa ushauri kwa uongozi.

Katika hatua nyingine, wanachama wa Yanga wameridhia kuwaongezea muda wa miaka miwili, wadhamini wa bodi ya klabu hiyo, Mama Fatma Karume na Francis Kifukwe.

Mbali na kuwaongezea muda viongozi hao, wanachama wamekubali kuongezwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika kuwa mjumbe mwingine wa bodi hiyo.

Mkuchika ataungana na Kifukwe na Mama Karume na wadhamini wengine wawili, watakaoongezwa hapo baadaye na kuunda bodi itakayokuwa na wadhamini saba

No comments:

Post a Comment